NA HAJI NASSOR

MTANDAO wa asasi za kiraia kisiwani Pemba (PACSO) umesema, unaamini wananchi wanahitaji kwa kiasi kikubwa kujua matumizi ya fedha za umma katika miradi lakini changamoto iliyopo ni kukosa fursa ya kushirikishwa.

Hayo yalielezwa na Mratibu wa mradi wa ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za umma, Mohamed Najim Omar, wakati akizungumza na wajumbe wateule wa ujazaji wa madodoso, yenye lengo la kujua kama wananchi wanaelewa na kushirikishwa kwenye matumizi ya fedha za umma.

Katika mkutano huo uliofanyika Chake Chake, Mratibu huyo aliwahakikisha wajumbe hao kuwa hawatapa tabu wakati wakiwahoji wananchi wa shehia za Chambani na Madungu, juu ya matumizi ya fedha za ujenzi wa skuli zao ulivyotumika.

Alisema, kila mwananchi ana hamu ya kutaka kujua juu ya matumizi na ushirikishwaji wao pale serikali au wafadhili wanapotaka kujenga vyumba vya madarasa katika maeneo yao.

 “Kila mwananchi anatamani kushirikishwa katika uanzishaji wa miradi kama ya skuli, sasa naamini mkienda hamtapata usumbufu mkubwa kwa sababu wako tayari kutoa taarifa hizo,”alieleza.