NA HAFSA GOLO

IKIWA mchakato wa kuwapata wagombea ubunge kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) unaingia katika hatua ya mwisho wiki hii, wapo baadhi ya watia nia watapenya na wengine watatoka katika kinyang’anyiro hicho.

Vikao hivyo vitapitia majina ya wagombea wapatao 10,000 kwa nafasi za uongozi kwa majimbo 264 kwa nafasi za wabunge na viti maalumu.

Pamoja na mambo mengine lakini vikao hivyo vitalazimika kutumia sifa za ziada ukiacha kuongoza kura za maoni ikiwamo mgombe kutokiuka maadili hasa kujihusisha na vitendo vya rushwa.

Kwa kuwa hapo awali kulikuwa na malalamiko mengi kupitia nafasi za uongozi majimboni na viti maalumu ni wazi kuwa vikao hivyo vitazingatia uhalali wa uteuzi kwenye vikao hivyo.

Bila ya shaka hatua hiyo itasaidia kuleta ustawi mwema na kuondokana na uvumi,vituko na lugha mbaya zinazoweza kuleta dosari katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.

Kama hivyo ndivyo, kupitia mchakato huo wa mwisho kutawafanya hata wapiga kura wa makundi yote kuwa na Imani na uteuzi huo.

Sina dhamira mbaya, wala kuonesha kidole kwa wagombea walioongoza majimbo hayo isipokuwa lengo ni kujenga chama mazingira bora endelevu sambamba na kutimiza malengo yake ya kuleta ushindi wa kishindo.

Ifahamike kwamba ushindi wa Chama chochote cha kisiasa  hupatikana zaidi kwa umoja na mshikamano sambamba na viongozi kuwa waadilifu, uchapakazi na wenye kutatua kero za wananchi zinazoikabili jamii.

Bado chama cha Mapinduzi ni chama kikubwa chenye hadhi na chenye kukubalika hapa Tanzania, Afrika na dunia kwa ujumla, hivyo suala la kuwapata wagombea wenye sifa kwa maslahi ya chama na taifa kwa jumla yatazingatiwa kwa staili yake.