NA MADINA ISSA

BENKI ya Watu wa Zanzibar (PBZ), imesaini mkataba wa kununua hisa za benki ya MUCOBA kwa asilimia 75 ili kuendeleza biashara kati ya benki hizo.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kusaini mkataba kati ya PBZ na MUCOBA, Mkurugenzi wa PBZ Iddi Haji Makame, alisema makubaliano hayo yataiwezesha benki hiyo kuimiliki benki hiyo.

Alisema kuwa benki ya MUCOBA katika kufanya faida imeyumba kutokana na kukosa uwezo wa kutomuhudumia mteja ambaye anahitaji kiasi kikubwa cha fedha.

“Mteja atataka fedha kiasi cha shilingi milioni 100 hadi milioni 200, uwezo huo huna hivyo kipindi hicho iliyumba kweli, ila PBZ kununua hisa itasaidia benki ya MUCOBA kuinuka tena kibiashara,” alisema.

Hata hivyo, alisema kuwa imani yao itakuwa rahisi kuiendeleza benki hiyo kwani utamaduni wao unalingana kwa ajili ya kuinua benki hiyo na kuweza kuinua mitaji pamoja na mifumo ya kibenki.

Sambamba na hayo, alisema kuwa faida itakayopatikana itarahisisha katika miamala ya kifedha ikiwa mteja atakuwa na kadi ya PBZ na MUCOBA ataweza kutumia benki hizo.

Naye Mwenyekiti wa bodi ya benki hiyo, Profesa Dominicus Kasilo, alieleza kuwa benki hiyo kwa kipindi kirefu ilitetereka kutokana na kukosa uaminifu wa wasimamizi jambo ambalo limesababisha kukosa fedha hasa za kuwakopesha wateja wao pamoja na kukosesha mikopo.

Aidha alisema, kwa wakati huo hawajasimamisha huduma kwani walitumia mbinu za kitaalamu kuwapata wanahisa wengine wa benki kwa kuwapelekea fedha za dharura ili kuweza kuwahudumia wateja wao.

Sambamba na hayo, alisema kuwa Benki ya watu wa Zanzibar wamekuwa wakifanya kazi kwa kutengeneza faida bila ya kumtegemea mtu, ambapo kwa sasa wamewekeza kwa kununua hisa katika benki na taasisis mbalimbali za fedha.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya PBZ, Kidawa Hamid Saleh, alisema makubaliano hayo yatasaidia kuimarisha huduma za kibenki katika mikoa ya Tanzania.

Benki ya MUCOBA imefunguliwa mwaka 1998 na kufanya kazi zake kama benki na ilipofika mwaka 2017 benki ilitetereka na baada ya kubaini ubadhilifu uliokuwepo waliweza mwishoni mwa 2018 na 2019 na kuweza kufanya kazi kwa lengo la kuwatafuta wawekezaji ili waweze kufanya kazi.