LEO hii wapenzi wasomaji wetu wa Zanziabrleo katika safu yetu hii ya maakuli nawaletea pishi mwanana la pizza ya samaki.

Pishi hili ni zuri na tamu hivyo jaribu kulipika siku moja nawe utaona.

VIFAA VINAVYOTUMIKA KUPIKA PISHI HILI

Tuna steki wa kopo (oiled)                                   180 – 185 g 

Tomato ya kopo (paste)                                          3 Vijiko vya supu

 Kitunguu maji                                                           1

 Chumvi                                                                    1 kijiko cha chai

 Unga wa ngano                                                        4 vikombe

 Mafuta ya zaituni                                                      Nusu kikombe

 Hamira                                                                    1 kijiko cha chai

 Cheese ya Pizza                                                        100 g

NAMNA YA KUTAYARISHA NA KUPIKA

 Katika bakuli kubwa tia unga, hamira,mafuta na chumvi.Kisha mimina maji kidogo kidogo hadi mchanganyiko uwe donge la kunata kiasi tu. 

Funika na uwache unga kwa muda wa nusu saa kisha ukande tena kiasi ukijipaka mafuta mikononi, ufinike kwa muda wa masaa manne hadi sita.

Ukishaumuka kufura itakuwa tayari kwa kuandalia vitu vya kuweka juu.

Mimina tuna kwenye sahani huku ukichambua kuzidisha vijipande pande.

Katakata kitunguu slesi nyembamba kando, tomato (paste) ndani ya kijibakuli tia maji vijiko 2 vya supu kisha koroga ili iwe kidogo nyepesi.

Pake siagi au mafuta kiasi katika treya utakayochomea.

Chukuwa unga ulioumuka ukande ufanye donge moja na limwagie unga mkavu.

Litandaze donge kwenye treya mpaka upate chapati kubwa kwa mikono bila kutumia kifimbo.

Mwagia tomato (paste) kwenye pizza utandaze, kisha tuna halafu tupia vitunguu na utamalizia na cheese.  

Choma kwenye oveni kwa moto wa 200°C kwa muda wa dakika 25.

Kisha unaweza kukata (shape) upendayo na itakuwa tayari kuliwa.

KIDOKEZO:

Ukipenda pilipili za kuwasha unaweza kuongezea na pia unaweza kutumia brokoli badala ya tuna. Ni vizuri kuliwa ikiwa moto moto.