NA FATMA KITIMA, DAR ES SALAM

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambae pia ni mgombea nafasi hiyo kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) Dk. John Pombe Magufuli anatarajia kuchukua fomu kuwania nafasi hiyo baadae wiki hii baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)kutangaza ratiba ya uchaguzi hivi karibuni.

Katibu wa Halmashauri kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi Humphrey Polepole, aliyasema hayo wakati akizungumza na Waandishi wa habari katika ofisi ndogo za CCM Lumumba jijini Dar es Salaam.

Alisema CCM ipo katika mchakato wa kujiandaa na uchaguzi mkuu na kwamba mgombea wao atachukua fomu ya kuwania kipindi cha pili cha miaka mitano katikati ya wiki hii katika ofisi za NEC jijini humo.

Katibu huyo aliwataka wanaCCM kutulia katika kipindi cha kusubiri mchakato wa kuwapata wagombea wa nafasi ya Ubunge, Uwakilishi na Udiwani na kuamini chama chao hakitawaangusha kwa wale wote waliotiliwa shaka kufanya vitendo vya rushwa.

Alifafanua kuwa katika mwaka 2016 chama hicho kupitia vikao vyake kikiwemo cha Halmashauri Kuu na Kamati Kuu kilifanya mageuzi makubwa ya oganaizesheni na uongozi na kukirudisha chama katika mstari.

“CCM kwa sasa tunataka viongozi waadilifu, wachapakazi, wanaochukia rushwa, tutawafundisha watu adabu, hii itakua fundisho kwa wengine na itabaki kwenye historia kulikua na watu wakubwa tu lakini tuliwashikisha adabu,” alisema na kuongeza kuwa wamepokea malalamiko mengi ya vitendo vya rushwa na bado wanaendelea kupokea.

Akizungumzia juu wimbo wa Taifa kubadilishwa maneno na chama cha demokrasia na maendeleo (CHADEMA), Pole Pole alisema inasikitisha kuona Chama hicho kimethubutu kuweka maneno binafsi, jambo ambalo linavunja sheria za nchi.

Akiendelea alisema nchi hii inatambulishwa na vitu vitatu ambavyo ni jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bendera ya Taifa na Wimbo wa Taifa, vitu ambavyo vinalipa hadhi taifa la Tanzania duniani kote.

“Tufanye siasa lakini tusiguse vitu vinavyotambulisha taifa letu wimbo wa taifa huwa tunaimba tukiwa katikati ya vita, mapigano na ndio kiunganishi chetu kimaombi kati ya taifa letu na Mwenyezi Mungu, waombe radhi Watanzania kwa kuushushia hadhi” alisema.

Alisema hoja inayojengwa na chama hicho ya kuhoji wapi walipovunja sheria, wakati wakijua katika nchi hii kuna sheria, hivyo alisema anawaachia Watanzania kukipima chama hicho kwani kabla ya kupata dhamana ya kuongoza nchi wamebadili wimbo wa taifa na kuufanya wa chama chao jambo linaloweza kufanywa kwa tunu nyengine za taifa.