NA ASIA MWALIM

JESHI la Polisi mkoa wa Mjini Magharibi linawashikilia watu wawili wanaodaiwa kujishughulisha na vitendo vya utapeli dhidi ya wananchi huku wakijisingizia wao ni maofisa wa jeshi hilo.

Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Awadh Juma Haji, alithibitisha kukamatwa kwa watu hao alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari huko ofisini kwake Mwembe Madema mjini Zanzibar.

Kamanda aliwataja watuhumiwa hao ni Ali Said Masoud (47) mkaazi wa Chuini ambae aliwahi kuwa askari polisi mwenye namba F.2941 cheo cha Constable, ambae alikua akifanya kazi kituo cha polisi Ng’ambo wilaya ya mjini, ambapo alifukuzwa kazi mwaka 2012 kwa kosa la ujambazi.

Alimtaja mtuhumiwa mwengine ni Salum Khatib Mkwende (43) mkaazi wa Miembeni ambae aliwahi kuwa askari wa jeshi la kujenga uchumi (JKU) mwenye namba MU.1932 cheo cha Private aliyefukuzwa kazi mwaka 2008 kwa kosa la utoro jeshini.

Alisema kuwa katika kutekeleza matukio ya utapeli watuhumiwa hao hupita kwenye nyumba za wageni hasa maeneo ya Fuoni na kuwavizia wanawake wanaotoka kwenye nyumba hizo kisha kuwatapeli fedha kwa kujitambulisha kuwa wao ni askari polisi.

Kamanda huyo alisema watuhumiwa hao huwalazimisha wananchi wawapatie fedha na wasipotoa huwatishia kuwafikisha kwenye vituo vya polisi kwa kujihusisha na biashara ya ukahaba.

Alifahamisha kuwa watuhumiwa hao kwa sasa sio waajiriwa tena kwenye serikali bali hufanya ubabaishaji na vitendo vya kihalifu kwa kujinadi kuwa wao ni askari.

Sambamba na hayo aliwataka wanawake kuondoa nidhamu ya woga pindi anapokuja mtu kujitambulisha kuwa ni Askari, anapaswa ahoji na kuuliza kosa lake la msingi ili kuepusha kurubuniwa kirahisi.

Aidha kamanda aliwataka wananchi kutoa taarifa kwa vyombo vya usalama ili kupunguza urahisi wa kutapeliwa na wasisite kukagua vitambulisho vyao vya kazi ili kubaini ukweli na kujiridhisha.