KUALA LUMPUR, MALAYSIA

POLISI  nchini Malaysia wameivamia ofisi ya kituo cha televisheni cha Al Jazeera na vituo vyengine viwili nchini humo, na kuchukuwa kompyuta kadhaa ikiwa sehemu ya uchunguzi juu ya filamu fupi inayoonesha wahamiaji haramu ambayo iliiudhi serikali.

Al Jazeera ambayo inamilikiwa na Serikali ya Qatar ilisema kwenye taarifa yake kwamba uvamizi huo ulifanyika juzi, na ililaani muendelezo wa ukandamizaji wa Serikali ya Malaysia dhidi ya uhuru wa habari.

Mwezi uliopita, polisi ilianza uchunguzi juu ya filamu hiyo inayoonesha madhila wanayotendewa wahamiaji haramu nchini Malaysia, baada ya maofisa wa Serikali kulalamika kwamba yalikuwa si ya kweli na inayoegemea upande mmoja.

Wafanyakazi kadhaa wa Al Jazeera walihojiwa na polisi kwa tuhuma za uchochezi na uzushi na kuvunja sheria ya mawasiliano na vyombo vya habari ya Malaysia.