NA KHAMISUU ABDALLAH

JESHI la Polisi Mkoa wa Mjini kwa kushirikiana na Kikosi cha Kuzuia Magendo (KMKM), linaendelea kumtafuta Juma wa Juma Makame mwenye umri wa miaka 73 mkaazi wa Mbweni aliyepotea tangu Agosti 19 mwaka huu katika pwani ya Mazizini.

Kamanda huyo wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Kamishna Msaidizi wa Polisi Awadh Juma Haji, alisema walipokea taarifa za kupotea kwa mtu huyo Agosti 19 mwaka huu baada ya familia yake kutoa taarifa.

Alisema jeshi la polisi lilifika katika eneo la tukio na kukuta gari yake yenye namba za usajili Z. 260 KN pamoja na nguo.

Alisema taarifa zilizopatikana ndani ya familia mtu huyo aliondoka nyumbani kwake majira ya saa 11:00 jioni kuelekea pwani Mazizini kwa ajili ya kufanya mazoezi ikiwa ni kawaida yake kila inapofika jioni kwenda mazoezi katika pwani hiyo.

“Mtu huyu ana nyumba mbili nyumba moja ipo Mbweni na nyengine Chukwani baada ya kuona kwa wake zake kote hajarudi ndipo walipoanza wasiwasi na kutoa taarifa kwetu,” alisema.

Hivyo aliwaomba wananchi wanaomfahamu kutoa ushirikiano wa taarifa ambazo zitaweza kulisaidia jeshi hilo.

Mmoja wa shuhuda wa tukio hilo, Talib Tamim ambaye ni mvuvi wa eneo hilo, alisema walimuona mtu huyo akiogelea, lakini hawajashughulikia umaliziaji wa zoezi lake.

Alisema, wakati anaogelea katika eneo hilo alikuwa peke yake na hakuna mkusanyiko wa watu.

Alisema walipata taarifa majira ya saa 2:00 usiku baada ya familia kwenda kumuulizia na kukuta gari na nguo zikiwa zipo katika maeneo hayo.

Naye, mtoto wake ambae hakutaka kutajwa jina lake gazetini alisema walipata wasiwasi baada ya baba yao kuchelewa kurudi nyumbani kwani ni kawaida yake sala ya Isha amekuwa akisali nyumbani.

“Tuna utamaduni wa baba yetu ikifika magharibi na isha lazima asali ndani tulipiga simu kwa mama wa nyumba ya Mbweni na alitwambia ameondoka kwenda mazoezi na baadae alisema atakwenda Chukwani ndipo tulipoanza wasiwasi na kuanza kumtafuta,” alisema.

Mkuu wa kikosi cha Kuzuia Magendo (KMKM), aliyekuwa anaongoza katika utafutaji wa mtu huyo, Muhidin Yassin alisema walifika katika eneo hilo majira ya asubuhi Agosti 20 na kufanya operesheni katika eneo hilo lakini mpaka sasa hawajaona kitu chochote.

Alisema maiti ikizama ndani ya masaa 12 inakwenda chini ya maji lakini wanapata wasiwasi kwamba mtu huyo amezama au la.

“Mtu akizama na maji yakitoka basi tungekuwa tumeshamuona lakini sasa tunapata wasiwasi kwamba ni kweli alizama au hajazama ndio tunaendelea na zoezi,”.

Hivyo, aliwaomba watu wanaokwenda kufanya mazoezi basi kufatana na watu ili linapojitokeza tatizo iwe rahisi kupata msaada na taarifa za uhakika.