NA FARIDA MSENGWA, MOROGORO

KAMANDA wa Polisi mkoani Morogoro, Wilbrod Mutafungwa amewaonya madereva wa malori kuwa makini na kuikagua mizigo yao kabla ya kuanza safari ili kuepusha ajali zinazoweza kuzuilika.

Akizungumza katika mkutano wake na waandishi wa habari kuzungumzia ajali ya Lori lililobeba kontena na gari ya Costa iliyotokea juzi maeneo ya NANENANE alisema ilisababishwa na dereva wa Lori ambaye hakuwa na umakini wa kukagua alichokibeba kama kiko salama kabla ya kuanza safari.  

Akizungumza na gazeti hili mmoja wa Majeruhi  aliyelazwa hospitali ya rufaa Morogoro aliyepanda Costa kuanzia Mdaula Edwin Edson,  alisema, walipofika katika eneo la Chuo Kikuu Cha Jordan NANENANE alishtukia wameaangukiwa na kontena na kufanya gari yao kugandamizwa.

Edson alisema anachoshukuru hakupoteza fahamu na alishuhudia namna kontena la lori lilivyo wakandamiza na baadhi ya waliokuwemo kwenye costa hilo walipopiga kelele na baada ya kufunikwa na lori wananchi walijiokuwa karibu walijitokeza kuwasaidia kwa kuwavuta.

Aidha alisema baadae watu waliokuwa wakiwasaidia wakiwemo viongozi wa serikali walifika na gari la kuinua kontena lilisaidia kuinua na kuondoa wale waliokuwa wamekaa viti vya mbele na kukimbizwa hospitali ya mkoa wa Morogoro kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Naye Steven Kabanga, ambaye ni kondakta wa Costa alisema yeye hakuona namna lori lilivyoanguka anachokumbuka ni kushtukia kubanwa na kontena na alizimia hapo hapo.

Kamanda Mutafungwa alisema, chanzo cha  ajali hiyo ni kukatika kwa kontena lililokuwa limebebwa na lori na kwamba vyuma vilivyoungwa kati ya lori na kontena havikuwa katika ubora ambapo alitoa taadhari kwa madereva kuhakikisha kabla ya kuanza safari zake kufanya ukaguzi.

Mutafungwa alisema baada ya kutokea kwa ajali hiyo walifika kwa wakati eneo la tukio na kuwaokoa majeruhi sita ambao ambao hali zao zilikuwa nzuri na majeruhi wengine wanne kuonekana hali zao kuwa mbaya ambapo wote kwa pamoja walikimbizwa katika hospitali ya rufaa mkoa wa Morogoro kwa matibabu zaidi.