LISBON, Ureno
KLABU ya PSG imekata tiketi ya kucheza hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1995, kufuatia ushindi wa magoli 2-1 dhidi ya Atalanta BC ya Italia.

PSG chini ya kocha Thomas Tuchels ilifunga magoli hayo katika dakika za lala salama na kuibuka na ushindi huo katika mchezo uliokuwa mkali wa robo fainali.
Atalanta ilikuwa ya kwanza kupata bao katika kipindi cha kwanza kunako dakika ya 27, lilifungwa na Mario Pasalic ambalo lilikuwa ni goli lake la 12 msimu huu kwenye michuano yote.

Lakini, magoli mawili ya PSG yalifungwa ndani ya sekunde 149 kupitia kwa Marquinhos mnamo dakika ya 89 na Choupo-Moting kunako dakika ya 93, yalitosha kuibeba PGS.
Mwamuzi, Anthony Taylor, aliongeza dakika tatu ambazo zilionekana kuivuruga Atalanta baada ya kuongoza kwa muda mrefu.

Mara ya mwisho PSG kucheza mchezo wa nusu fainali ya michuano hiyo ilikuwa msimu wa 1994-95 chini ya kocha Luis Fernandez ambapo walipambana na AC Milan na walitolewa kwa kufungwa jumla ya magoli 3-0 kwenye mchezo wa mikondo miwili.

Katika hatua ya nusu fainali, PSG itacheza na mshindi wa mchezo mwengine wa robo fainali kati ya RB Leipzing na Atletico Madrid uliotarajiwa kuchezwa jana usiku.
Atalanta: Sportiello, Toloi, Caldara, Djimsiti, Hateboer, de Roon, Freuler, Gosens, Gomez, Pasalic na Zapata.

PSG:Navas, Kehrer, Thiago Silva, Kimpembe, Bernat, Herrera, Marquinhos, Gueye, Icardi, Neymar na Sarabia.(AFP).