MINSK,BELARUS

RAIS  wa Belarus Alexander Lukashenko amesema  kuwa rais wa Urusi Vladimir Putin ameahidi kutoa msaada wa ulinzi kwa nchi yake wakati taifa hilo linakabiliwa na wimbi la maandamano yaliyochochewa na matokeo ya uchaguzi mkuu.

Lukashenko anayeandamwa na changamoto kubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa tangu alipochukua madaraka mwaka 1994, alizungumza kwa njia ya simu na Rais Putin aliyeahidi kutoa msaada mkubwa wa ulinzi kwa Belarus.

Maelfu ya Raia wa Belarus wanapanga kufanya maandamano makubwa  baada ya kujitokeza kwa wingi kwenye mji mkuu, Minsk, kuitikia wito wa mgombea urais wa Upinzani anayedai kulikuwa na wizi wa kura katika uchaguzi wa wiki iliyopita.

Katika uchaguzi huo Lukashenko alitangazwa mshindi kwa zaidi ya asilimia 80, lakini upinzani uliyapinga matokeo na kumtaka kiongozi huyo kujiuzulu na kisha uchaguzi mpya ufanyike.