BAMAKO,MALI

MAELFU ya waandamanaji wa upinzani wamerejea tena katika maandamano nchini Mali, kushinikiza kujiuzulu kwa Rais Ibrahim Boubacar Keita na Waziri mkuu wake Boubou Cissé.

Ujumbe na maneno yaliyoandikwa kwenye mabango yanayobebwa na waandamanaji hao yanamlenga Rais Keita, ambaye yuko madarakani tangu 2013, lakini pia Waziri Mkuu wake Boubou Cissé.

Haya ni maandamano ya kwanza dhidi ya utawala tangu mrengo wa upinzani nchini Mali usitishe maandamano yake Julai 21 kufuatia maadhimisho ya sikukuu ya Eidul-Adh’ha.

Wakuu wa Serikali kutoka Jumuiya ya Uchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) waliingilia kati mgogoro huo, ambapo tarehe 27 Julai walipendekeza kuundwa Serikali mpya itakayojumuisha pia wanachama wa upinzani, sambamba na kumbakisha Keita katika nafasi yake ya urais.

Mbali na hatua nyengine, viongozi hao wa ECOWAS walimuhimiza Rais Keita ateue pia majaji wapya wa Mahakama ya Katiba ili kuutatua mzozo uliopo kuhusu matokeo ya uchaguzi.

Harakati ya upinzani nchini Mali ya Juni 5 ilisisitiza mara kadhaa kuwa haikubaliani na pendekezo hilo la viongozi wa ECOWAS na kuendelea kushikilia msimamo wake wa kutaka Rais Keita ajiuzulu.

Kwa sehemu kubwa, mgogoro unaoendelea sasa nchini Mali ulichochewa na hatua iliyochukuliwa na Mahakama ya Katiba mwezi Aprili mwaka huu ilipofuta matokeo ya uchaguzi wa bunge uliokuwa ukisubiriwa kwa muda mrefu wa majimbo 30, hatua ambayo ilikinufaisha chama cha Rais Abubakr Keita.