BAMAKO,MALI
RAIS wa Mali Ibrahim Boubacar Keita ametangaza kujiuzulu kupitia televisheni, masaa machache baada ya wanajeshi kumkamata na Waziri wake mkuu, Boubou Cisse, katika mji mkuu, Bamako.
“Nimeamua kuachia nafasi yangu”, alisema Keita kupitia kituo cha utangazaji cha taifa ORTM.
Awali picha na vidio zilizosambaa mitandaoni zilionesha msafara unaoaminika kuwa wa Rais Keita na Waziri Mkuu Cisse uliokuwa umezingirwa na wanajeshi.
Wanajeshi hao walianza uasi katika mji wa Kati, uliopo umbali wa kilomita 15 kutoka Bamako,ambapo milio ya risasi ilisikika.
Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS), Umoja wa Mataifa,Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika zimelaani uasi huo na kuonya juu ya jaribio lolote la kubadili madaraka kinyume na katiba. Mali ilikuwa ikijaribu kurejesha utulivu tangu maelfu ya wafuasi wa upinzani walipoingia barabarani wakimtuhumu Keita kwa ufisadi na kudhoofika kwa usalama katika eneo la kaskazini linalokabiliwa na mashambulizi ya wapiganaji wa siasa kali.