BAMAKO,MALI

RAIS  Ibrahim Abubakar Keita wa Mali ameteua majaji tisa wa Mahakama ya Katiba kwa kutumia mamlaka ya urais ikiwa ni sehemu ya hatua ya maridhiano inayolenga kupoza joto la mgogoro wa kisiasa unaoendelea nchini humo kwa miezi kadhaa sasa.

Taifa hilo la eneo la Sahel limetingwa na mkwamo wa kisiasa unaomuhusisha Rais Keita na upinzani unaomshinikiza ajiuzulu.

Watu 11 waliuawa mwezi uliopita wa Julai katika machafuko yaliyoendelea kwa zaidi ya siku tatu kufuatia maandamano ya upinzani dhidi ya kiongozi huyo, kutokana na mgogoro mbaya wa kisiasa kushuhudiwa nchini Mali kwa miaka kadhaa.

Wakuu wa Serikali kutoka Jumuiya ya Uchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) waliingilia kati mgogoro huo, ambapo tarehe 27 Julai walipendekeza kuundwa Serikali mpya itakayojumuisha wanachama wa upinzani,sambamba na kumbakisha Keita katika nafasi yake ya urais.

Mbali na hatua nyengine,viongozi hao wa ECOWAS walimuhimiza Rais Keita ateue  majaji wapya wa Mahakama ya Katiba ili kuutatua mzozo uliopo kuhusu matokeo ya uchaguzi.

Harakati ya upinzani nchini Mali ya Juni 5 ilisisitiza mara kadhaa kuwa haikubaliani na pendekezo hilo la viongozi wa ECOWAS na kuendelea kushikilia msimamo wake wa kutaka Rais Keita ajiuzulu.

Ofisa katika ofisi ya Rais ambaye hakutaka jina lake litajwe aliviambia vyombo vya habari kuwa, majaji tisa walioteuliwa wataapishwa leo, Hata hivyo upinzani ulisema, umeshaandaa maandamano mengine makubwa ya nchi nzima dhidi ya Rais Keita ambayo yatafanyika siku ya kesho.

Kwa sehemu kubwa, mgogoro unaoendelea sasa nchini Mali ulichochewa na hatua iliyochukuliwa na Mahakama ya Katiba mwezi Aprili mwaka huu ilipofuta matokeo ya uchaguzi wa bunge uliokuwa ukisubiriwa kwa muda mrefu wa majimbo 30, hatua ambayo ilikinufaisha chama cha Rais Abubakr Keita.