KAMPALA,UGANDA

RAIS Yoweri Museveni wa Uganda  ameteua kamati ya kusimamia hatua za udhibiti wa virusi vya Corona huku idadi ya maambukizi na vifo ikiongezeka nchini humo.

Akizungumza kupitia televisheni,Waziri wa Afya nchini humo Ruth Aceng alisema kamati hiyo inayoongozwa na ofisa wa ngazi ya juu wa jeshi itasimamia maelekezo yote ya utaratibu maalumu wa utendaji yaliyotolewa na Rais wa nchi hiyo pamoja na Wizara ya afya.

Alisema timu hiyo inayojumuisha wajumbe kutoka Wizara ya afya, vyuo vikuu,polisi na jeshi, itasimamia ugawaji wa barakoa nchini humo na kusimamia matumizi sahihi ya barakoa hizo katika jamii.

Kamati hiyo inaundwa wakati nchi hiyo ikishuhudia kuongezeka kwa idadi ya kesi za maambukizi ya virusi vya Corona,ambapo mpaka kufikia Agosti 13, kulikuwa na kesi 1,353 zilizothibitishwa,huku wagonjwa 1,141 wamepona na 11 kufariki.