NA MZEE GEORGE
MKUU wa Mkoa Mjini Magharib, Hassan Khatib Hassan ameuomba uongozi wa Jumuiya ya watu wa Pakistani wanaoishi Zanzibar kudumisha umoja na mashirikiano yaliopo baina wananchi wa Pakistani na Zanzibar.
Hassan alitoa ombi hilo katika hafla ya sherehe ya siku ya uhuru wa Pakistani kutimia miaka 74 zilizofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Africa House iliyopo Shangani Mjini unguja.
Alisema mashirikianao yaliopo baina ya wananchi wa Zanzibar na wapakistani waishio nchini yanafaa kuendelezwa kwa maslahi ya pande zote mbili.
“Tumekuwa na wananchi wa mataifa mbali mbali katika nchi yetu mkiwemo nyinyi raia wa Pakistani na tumekuwa tukishirikiana katika mambo mabli mbali ikiwemo biashara, hivyo mashirikiano na ukaribu huu uendelee”, alisema Hassan.
Aidha Mkuu wa Mkoa aliuomba uongozi huo kuunda urafiki wa kitamaduni kati ya baraza la manispaa moja liliopo Mkoa wa Mjini Magharibi na liliopo Pakistani katika kubadilishana uzoefu na kusaidia wananchi wa Mkoa huo kwa sekta tofauti ikiwemo elimu na biashara.
Mkuu huyo alitumia hafla hiyo kuwahakikishia wananchi na wanajumuiya wa Pakistani wanaoishi Zanzibar kuishi kwa amani na usalama kwa muda wote wakati nchi ikielekea katika uchaguzi mkuu na baada ya uchaguzi.
Mapema Mwenyekiti wa Jumuiya ya wapaikistani wanaoishi Zanzibar, Shakil Ahmed alisifu ukarimu wa wananchi na viongozi wa Tanzania ikiwemo Zanzibar na kuiweka nchi katika hali ya amani na utulivu.
Alisema jitihada zinazochukuliwa na viongozi wa serikali kupitia chama cha mapinduzi ni zakupigiwa mfano na mataifa mbali mbali na kupelekea wao kusherehekia uhuru wa nchi yao kwa kutimia miaka 74 kwa Amani.
“Tunapongeza uongozi wa serikali ya CCM kwa kusimamia amani na maendeleo ya nchi hii, tumekuwa tunawaalika viongozi wakuu wan chi hii katika sherehe zetu mbali mbali za uhuru na tunawapata bila matatizo na hapa ndio tunaona ukarimu wa wananchi wan chi hii’alisema mwenyekiti huyo.
Aliongeza kuwa jumuiya yao ndio mara ya kwanza kufanya sherehe hizo kwa visiwani Zanzibar na kwamba mwakani wanakusudia kufanya shughuli mbali mbali za kijamii ikiwemo kuwatembelea wagonjwa na mambo mengine kabla ya kupata chakula cha usiku.