NA MADINA ISSA

MKUU wa Mkoa wa Kusini Unguja, Ayoub Mohammed Mahmoud, amewataka wazazi na walezi kuendeleza ushirikiano na walimu ili kuhakikisha watoto hao wanapata elimu kwa ufanisi.

Aliyasema hayo alipokuwa katika mahafali ya kwanza kwa wanafunzi waliofaulu kidato cha pili katika skuli ya Ghana wilaya ya Kati mkoa wa Kusini Unguja.

Alisema ushirikiano unaweza kutatua changamoto zinazowakabili wanafunzi pamoja na kufanikisha malengo ya walimu na kuendeleza ufaulu kwa kiwango kikubwa wakati wa mitihani ya taifa.

Alisema, kamati ya maendeleo ya elimu ya shehia ya Ghana imefanya kazi kubwa ya kuhakikisha inaanza ujenzi wa madarasa mengine mapya ili kusudi kuhamasisha wengine kuchangia ujenzi wa madarasa hayo.

Hivyo, aliwataka wananchi kuchangia katika miradi ya kijamii ikiwemo ujenzi wa madarasa katika skuli hiyo.

Sambamba na hayo alisema atawashauri wamiliki wa viwanda vya kokoto,viwanda vya matofali na mashimo ya fusi waliopo katika mkoa huo kuchangia malighafi hizo ili ziweze kuendeleza ujenzi wa madarasa hayo.

Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa mkoa alitaka wazazi kuwafichua watu wanaowapa ujauzito wanafunzi ili wachukuliwe hatua za kisheria.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya maendeleo ya elimu katika shehia ya Ghana, Ali Mohammed Othman alisema kamati yake imefanikiwa kuongeza mwamko juu ya masuala ya elimu kuongeza ufaulu wa wanafunzi.

Alisema katika skuli yao waliweka kambi za wanafunzi wanaotarajiwa kufanya mitihani ya taifa pamoja na kuanzisha ujenzi wa vyumba vya madarasa mapya na kuongeza nafasi za kujisomea.

Naye mfanyabiashara, Said Nassir Bopar, katika hatua ya kuunga mkono juhudi za serikali za kuinua sekta ya elimu, aliahidi kuisaidia skuli hiyo mabati 150 kwa ajili ya kuezekea mabanda yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi.

“Sambamba na mabati hayo, pia nitawapatia kompyuta tano ili ziongeze ufanisi kwa walimu na wanafunzi katika mitihani yao na kazi za kila siku,” alieleza Bopar.

Asilimia 79.29 ya wanafunzi wote wa kidato cha pili waliofanya mitihani ya taifa katika skuli hiyo, walifaulu na kuendelea na kidato cha tatu huku skuli hiyo ikikabiliwa na changamoto za uhaba na uchakavu wa majengo na kukosekana kwa hatimiliki za maeneo ya skuli hiyo.