NA MADINA ISSA

MKUU wa Mkoa wa Kusini Unguj, Ayoub Mohammed, amewataka wazazi na walezi kuendelea kushirikiana na walimu ili kuweza kupata matokeo mazuri kwa wanafunzi na baadae kuja kupata viongozi waliokuwa na uwezo.

Akizungumza katika sherehe ya kuwakabidhi zawadi wanafunzi wa skuli ya Mapinduzi iliyopo Chaani Mkoa wa Kaskazini Unguja, waliofanikiwa kuendelea na kidato cha tano baada ya kufanya vizuri katika mtihani wa kidato cha nne.

Alisema endapo mashirikiano yataendelezwa yatasaidia kuondoa changamoto hizo kuwafanya walimu waongeze juhudi za ufundishaji.

Aidha alisema kuwa juhudi za pamoja zinahitajika kati ya walezi,walimu na wanafunzi, ili kuweza kutatua changamoto za kielimu kwa lengo la kuongeza kiwango cha ufaulu maskulini.

Alisema kutokana na kuongezeka kwa ufaulu ndani ya skuli hiyo ni vyema kuengeza hamasa na kutoa ushirikiano kwa wanafunzi wanaotarajia kufanya mitihani kwa kuwahimiza kusoma kwa bidii, ili kuhakikisha kiwango hicho kinaongezeka kwa asilimia kubwa.

Hata hivyo, aliwataka wanafunzi waliofanikiwa kuendelea na kidato cha tano kuongeza juhudi, ili waweze kufanya vizuri katika mitihani yao inayofuatia huku akiwataka wanafunzi wanaotarajia kufanya mitihani ya kidato cha nne mwishoni mwa mwaka huu kusoma kwa bidii, ili waweze kupata ufaulu mzuri.

Sambamba na hayo alisema kupitia kwa wahisani wa maendeleo ya kielime atahakikisha wanajenga madarasa manne, ili kuondoa uhaba wa madarasa katika skuli hiyo pamoja na kupatiwa chakula kwa ajili ya wanafunzi wanaokaa kambi kwa lengo la kujiandaa na mitihani yao ya taifa.