LONDON, England

MESUT OZIL, amezima tetesi zilizokuwa zikimhusisha kwamba anaweza kuondoka Arsenal, kwa kufichua kwamba atamalizia taaluma yake ya soka Emirates.

Ozil alipinga uwezekano wowote wa kuagana na Gunners kwa kushikilia kwamba, ataondoka klabu hiyo baada ya mkataba wake kufikia tamati Juni 2021, licha ya tofauti zake na kocha Mikel Arteta.

Mzawa huyo wa Ujerumani mwenye miaka 31, ambaye hupokea mshahara wa pauni 350,000 kila wiki, alisema anaweza kuwa wa msaada katika klabu hiyo ya London endapo atapewa nafasi.

 Kuhusu kukataa kupunguziwa mshahara kutokana na makali ya janga la virusi vya corona, Ozil alisema anaamini kwamba watu fulani wamekuwa wakijaribu kwa miaka miwili kumharibia jina.

Ozil alisema kama wachezaji, walitakiwa kupewa taarifa zaidi huku maswali yao yakikosa kujibiwa.

Matamshi ya Ozil yanakujia siku chache baada ya kuonekana pamoja na kocha wa Istanbul Basaksehir, Okan Buruk na kuibua fununu kuwa nguli huyo alikuwa kwenye harakati za kuondoka Arsenal.

Kiungo huyo wa kati kwa sasa anajivinjari nchini Uturuki na aliruhusiwa kuondoka Uingereza wakati Arsenal ilikuwa inavaana na Chelsea kwenye fainali ya Kombe la FA.