NA ASIA MWALIM

SEREKALI imeshauriwa kuongeza adhabu kwa madereva wanaotiwa hatiani kwa makosa ya usalama barabarani, ili kupunguza ajali za mara kwa mara zinazojitokeza nchini.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja ACP, Awadh Juma Haji, alitoa ushauri huo alipokua akizungumza na Zanzibar Leo, huko ofisini kwake Mwembemadema Mjini Unguja.

Kamanda alisema kuwa, jitihada ambazo zinachukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia jeshi hilo ni kubwa, lakini nguvu ya adhabu inahitaji kuongezewa kwa madereva hao kutokana na kuongezeka kwa matukio yao.

“Serikali yetu inachukua hatua nzuri kupambana na kesi hizi, tunashukuru kwani sheria zimewekwa vizuri lakini kuna haja ya adhabu kuongezwa” alisema kamanda.

Alifahamisha kuwa adhabu zinazotolewa ni ndogo na hazimfundishi mkosaji ukilinganisha kiwango cha pesa na wakati uliokuwepo, hivyo watuhumiwa hawaoni tabu kurejea makosa yao, baada ya kulipishwa faini ndogo.

“Kama mtu atapigwa faini ya shilingi 10,000 kwa karne hii tuliyonayo sasa haisaidii chochote, haoni tabu kufanya tena kosa hilo kutokana na faini yenyewe” alisema.