NA MARYAM HASSAN

MSHITAKIWA aliyedaiwa kumbaka mtoto wa miaka saba kwa siku mbili tofauti, amepelekwa rumande hadi Agoti 12 mwaka huu.

Mshitakiwa huyo ni Mohammed Makame Abdalla (20) mkaazi wa Kiboje, amefikishwa katika mahakama ya mkoa Mwera mbele ya Hakimu Saidi Hemed Khalfan.

Kwa mujibu wa maelezo ya wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Sara Omar Hafidh, alidai kwamba mshakiwa alipatikana na makosa hayo ambayo anadaiwa kutenda kwa siku tofauti.

Sara alisema kwamba, baina ya mwezi wa nne na wa tisa mwaka jana muda usiojulikana huko Kiboje uwandani, mshitakiwa alimuingilia kimwili mtoto wa kike mwenye umri wa miaka saba (jina linahifadhiwa).

Aidha mwezi huo huo, pia anadaiwa kumuingilia kunyume na maumbile mtoto huyo, huku akijua kuwa kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Aliposomewa shitaka lake mshitakiwa huyo alikataa na kuiomba mahakama kumpa dhamana, jambo ambalo lilikataliwa na upande wa mashitaka.

Sara alisema, makosa aliyoshitakiwa nayo mshitakiwa hayana dhamana na tayari upelelezi wake umekamilika, hivyo aliomba kuahirishwa kwa kesi hiyo na kupangwa kusikilizwa mashahidi.

Hivyo kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 8 mwaka huu kwa kuanza kusikilizwa mashahidi na mshitakiwa amepelekwa rumande.