MOSCOW,RUSSIA
WAZIRI wa Afya wa Russia Mikhail Murashko amesema kuwa majaribio ya chanjo ya corona yamekamilika nchini humo.
Alisema kuwa chanjo hiyo ya virusi vya corona ambayo ilitengenezwa na Taasisi na Kituo cha Taifa cha Utafiti wa Vijidudu Maradhi na Kudhibiti Magonjwa cha Gamalia tayari imekamilisha majaribio.
Waziri wa Afya wa Russia alieleza kuwa zoezi kubwa la utoaji chanjo dhidi ya virusi vya corona litaanza nchini humo kuanzia mwezi Oktoba.
Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo pia ilitangaza kuwa uchunguzi uliofanywa kwa watu watakaopatiwa chanjo hiyo ya corona unaonyesha namna chanjo hiyo ilivyo na kinga kamili ya virusi hivyo.
Inatarajiwa kuwa uzalishaji wa chanjo hiyo ya kwanza kutengenezwa na Russia utaanza mwezi Septemba mwaka huu.
Takwimu rasmi zilizotangazwa na Russia zinaonyesha kuwa, hadi sasa jumla ya watu 828,990 waliambukizwa corona nchini humo, na wengine 13,673 walifariki kwa maradhi ya Covid-19.
Serikali ya Russia katika wiki za karibuni imeliweka katika ajenda yake ya kazi suala la kutekeleza karantini nchini humo ili kukabiliana na maambukizi ya corona.