KIGALI,RWANDA

WIZARA inayosimamia masuala ya dharura (MINEMA) nchini Rwanda, imesema inathibitisha tena kanuni ya kurudisha kwa hiari wakimbizi,kulingana na sheria za kimataifa na Rwanda.

Hatua hiyo ilionekana kama ni suluhisho la kudumu nchini humo.Wizara ilitoa taarifa hiyo kufuatia rufaa ya wakimbizi zaidi ya 330 wa Burundi ambao walimwomba Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye wakitaka warudishwe kwa heshima na halali katika nchi yao.

“Rwanda inajitolea kuwalinda wakimbizi katika eneo lake,na iko tayari kuwarudisha salama na heshima  wale ambao hutaka kurudi kwa kushirikiana na shirika la  UNHCR  lililopewa jukumu la kulinda wakimbizi na Serikali husika,” taarifa ilieleza.

“Tunataka mazungumzo ya pande mbili kati ya Burundi na Rwanda mbele ya UNHCR ili tuweze kupata haki na heshima na kurudi nyumbani,” walisema katika maombi yao.

Emmanuel Bizimana, na Celeus Hatungimana, miongoni mwa waliosaini ombi hilo waliliambia gazeti la New Times kwamba walikimbia kwa sababu ya mzozo wa kisiasa na ukosefu wa usalama uliotokana na shitaka la Rais wa zamani wa Burundi, Pierre Nkurunziza wa kutumikia kipindi cha tatu kwa ubishani.

Kifungu cha 17 cha sheria inayohusiana na wakimbizi ambayo ilitungwa  2014 inatoa masharti sita ya kukomesha hali ya wakimbizi.

Takwimu kutoka UNHCR zinaonyesha kuwa Rwanda inakaribisha wakimbizi wapatao 77,000 kutoka DRC, na wakimbizi 71,000 kutoka Burundi wengine kutoka katika kambi na mijini.

Kwa mujibu shirika la UNHCR, mvutano unaohusiana na uchaguzi katika nchi jirani ya Burundi, Rwanda ilifungua mpaka wake kwa wakimbizi wa Burundi ambao walikimbia nchi tangu Aprili 2015.

Kambi ya Wakimbizi ya Mahama iliyopo Wilaya ya Kirehe katika Mkoa wa Mashariki imekuwa kambi kubwa zaidi nchini kwa kuwakaribisha wakimbizi wa Burundi na kwa sasa ina idadi ya wakimbizi karibu 60,000.