KIGALI,RWANDA

RWANDA imetoa waranti wa kumtia mbaroni Aloys Ntiwiragabo Mkuu wa zamani wa Intelijinsia wa nchi hiyo ambaye yuko chini ya uchunguzi hivi sasa nchini Ufaransa kwa kuhusika katika mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 huko Rwanda.

Aloys Ntiwiragabo

Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Rwanda Aimable Havugiyaremye, alisema kuwa,maofisa husika wa nchi hiyo walichunguza kesi ya mshukiwa huyo na sasa wanashirikiana na kikosi cha kupambana na jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu cha Ufaransa.

Ufaransa ilianza kuchunguza tuhuma za jinai dhidi ya binadamu zinazomuhusu Ofisa huyo wa zamani wa jeshi la Rwanda baada ya kukutwa katika kitongoji kimoja cha mji wa Orleans umbali wa kilomita 100 kusini magharibi mwa Paris.

Tovuti ya habari za kiuchunguzi ya Ufaransa inayoitwa Mediapart ndiyo iliyomfichua Ntiwiragabo ambaye alitajwa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kuwa mmoja wa wapangaji wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda.

Taarifa za mahali alipokuwa amejificha mkuu huyo wa zamani wa Intelijinsia wa Rwanda ziliwekwa wazi ikiwa imepita miezi miwili sasa tangu kutiwa mbaroni Felicien Kabuga mtuhumiwa mwengine wa mauaji ya kimbari ya Rwanda katika kitongoji kimoja cha Paris.