Nyimbo zake kivutio cha mashabiki wa umri tofauti
Amewashauri wasanii kupendana, kudumisha muziki huo

ZASPOTI

KILA lilopangwa kwangu Si aibu kunifika
Hakika si kosa langu Mola ameshaandika
Atakalo liwe kwangu Siwezi kuliepuka
Yote alonipa Mungu Mimi nimesharidhika

Katu si uwezo wangu Kufanya ninalotaka
Wivu wa nini wenzangu Roho juu kujiweka
Kilicho kwangu ni change Ni muhali kutoweka
Ni ridhaa yake Mungu Mjae kumtunuka”

Hii ni moja ya beti ya nyimbo maarufu ambayo ilighaniwa na muimbaji maarufu mwenye sauti ya kumtoa nyoka pangoni si mwengine, ni bibie Sabah Muchacho alipokua na kundi la East African Melody.
Msanii huyo ambae amefanikiwa kujizolea sifa katika sehemu mbali mbali duniani kupitia na nyimbo zake alizoziimba akiwa na vikundi mbali mbali na kumfanya awe maarufu na kuitangaza vyema sanaa ya muziki wa taarab ulimwenguni kote.


Jina lake halisi ni Sabah Khamis Said Bagmesh, lakini, sio wengi wala sio jina maarufu ambalo linajulikana na watu wengi isipokuwa ni wanafamilia na watu wa karibu na msanii huyo.
Wengi wao humfahamu kwa jina la Sabah Muchacho ambapo kama utakwenda sehemu yoyote na kutaja jina hilo basi uhakika moja kwa moja watakwambia ni la msanii wa muziki wa taarab


Kubatizwa kwa jina la Sabah Salum kunatokana na jina la mume wake, na jina la Muchacho linatokana na umaarufu wa kaka zake ambapo katika jiji la Dar es Salaam kama utataja jina hilo moja kwa moja utapelekwa katika familia hiyo kutokana na umaarufu walionao na kaka zake hao kuwa ni mashabiki wakubwa wa klabu ya soka ya Simba.


Nilipotaka kujua historia ya msanii huyo jinsi alipoanzia kuhusiana na maswala ya kujitumbukiza kwake katika fani hiyo na mpaka alipofikia hakukataa alinipa mashirikiano makubwa mpaka mwisho wa mazungumzo yetu.
Kama kawaida ya wasanii wengi wanavyoanzia na Sabah nae alikuwa hivyo hivyo kipaji chake cha uimbaji kilianzia tangu akiwa mdogo wakati anasoma madrasa alikua akighani kasida na skuli alikua akiimba nyimbo mbali mbali ikiwemo kwaya.


“Mimi fani hii sikurithi, hakuna mzazi wangu hata mmoja aliyekuwa muimbaji nakusudia baba yangu wala mama yangu haya yalikua mapenzi yangu mwenyewe tena nilianza masuala haya tangu nilipokua nasoma”, alisema.


Mnamo mwaka 1984, alijiunga rasmi katika ulimwengu wa taarab akiwa na kundi zima la ‘Mamesh’ lenye maskani yake jijini Dar es Salaam lililokuwa likimiliwa na Ahmed Azan ambapo akiwa anaingia ndani ya kundi hilo alianza kuwa muitikiaji na baadae alitungiwa nyimbo na kuimba mwenyewe.


Sabah anasema akiwa ndani kundi la Mamesh anakumbuka alitungiwa nyimbo mbili ambazo aliimba yeye mwenyewe alilozitaja kwa majina ya ‘Uongo na nyengine Ushoga una matata’.
Akiwa ndani ya kundi hilo alikutana na wasanii mahiri akiwemo Khamis Mzinga, Juma Nambe, Abdulshakur, Abdulrahman Muchacho wote hao marehemu wengine ni Mwanaid Shaaban na Salum Abdu ambae ni mume wake.


Sabah anasema, mwaka 1988, familia yake wakiwemo kaka zake, Ebrahim na Abdulrahman hao kwa sasa ni marehemu na mume wake pamoja na yeye mwenyewe walianzisha kundi lao linalojulikana ka jina la ‘All Star Modern Taarab’.


Anasema baaadhi ya wasanii kutoka Mamesh pia waliwafuata na kujiunga na kundi hilo la All Stars wakiwemo Juma Nambe na Abdulshakur, lakini, pia wasanii wengi walijiunga na kundi hilo akiwemo marehemu Leyla Khatib na wasanii wengi wengi chipukizi walijifundisha wakiwa na kundi hilo.


Aliwataja wasanii hao pamoja na Thabit Abdul, Amour Zungu, Mariam Alawi, Rajab Kondo, Ali J, Shariff na wasanii wengi walishiriki kuliinua kundi hilo ambalo lilionekana kuvuta mashabiki wengi wa jiji la Dar es Salaam na mikoa mengine.

INAENDELEA TOLEO LIJALO