Aling’ara Zanzibar Heroes kwa miaka 13 mfululizo
Asema, soka limempa mafanikio katika maisha yake


ZASPOTI

JINA la Said Kuzu sio geni ndani ya masikio na akili za mashabiki wa soka visiwani Zanzibar na Tanzania Bara kwa ujumla kutokana na umahiri wake aliokuwa nao wakati wa enzi zake.
Ni miongoni mwa majina makubwa yaliotamba katika klabu mbali mbali na kufanikiwa kuliweka jina lake katika ramani nzuri ya mchezo huo.

JINA la Said Kuzu sio geni ndani ya masikio na akili za mashabiki wa soka visiwani Zanzibar na Tanzania Bara kwa ujumla kutokana na umahiri wake aliokuwa nao wakati wa enzi zake.
Ni miongoni mwa majina makubwa yaliotamba katika klabu mbali mbali na kufanikiwa kuliweka jina lake katika ramani nzuri ya mchezo huo.


Jina lake kamili ni Said Mohammed Said, lakini, kama utafika katika maeneo ya Mji Mkongwe na sehemu nyengine na kumuulizia hutoweza kumpata na zaidi utapelekwa kwa mtu mwengine mpaka utaje jina la ‘Kuzu’.


Jina la Kuzu limetokana na umaarufu wa baba yake mzazi ambae alikuwa mchezaji wa mpira katika timu mbali mbali ikiwemo Miembeni, Jeshi pamoja na timu ya Taifa ya Zanzibar.
“Mchezo wa soka nimerithi kutoka kwa baba yangu mzazi na yeye ndio mwenye jina la umaarufu la ‘Kuzu’, yeye kacheza mpira na mimi nilipoingia katika fani hiyo ndio jina nikabatizwa na mimi”, alisema.


Kama kawaida ya wanasoka wengi wanaanza kucheza soka tangu wakiwa na umri mdogo, na yeye ndivyo alivyoanzia katika timu za watoto hivyo kutokana na kupenda mchezo huo, mwaka 1995 alijiunga na timu ya Forodhani Sports Club.


Hamu ya kuwa mchezaji mahiri ilionekana kutawala kwenye akili ya mchezaji huyo na ilipofika mwaka 1998 alijiunga na Mlandege ambapo huko alikutana na wachezaji mbali mbali akiwemo Haji Mwinyi, Shem Frank, Ramadhan Kidilu, marehemu Rifat Said na wengine wengi.


Kuzu alidumu na kikos hicho mpaka mwaka 2004 na kujiunga na klabu ya Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) ambapo alidumu kwa muda wa mwaka mmoja na kukutana na wachezaji aliowataja ni pamoja na Khamis Wawingwi, Mgaza Kinduli, Abdulhalim Humoud na wengineo.
Kutokana na kipaji chake kuvutia klabu mbali mbali, viongozi wa klabu ya Caps United inayoshiriki Ligi Kuu ya Zimbabwe walimvuta ambapo alicheza kwa msimu mmoja na baadae kurudi nyumbani na kujiunga tena JKU.


Mwaka 2008, Kuzu alihamia Miembeni ambapo alidumu na kikosi hicho kwa miaka saba na kusema alipofika huko alikutana na wachezaji mbali mbali akiwemo Amri Kiemba, Thomas Morris, Mohammed Golo,Samson Mwamanda na Lulanga Mapunda.
Anasema, mwaka 2014 hadi 2015 alihamia KMKM ambapo aliwataja wachezaji alikutana nao kwenye kikosi hicho ni pamoja na Ame Kibobea, Juma Kizungu, Mudrik Muhibu, Said Khalid na wengine wengi.


Kiwango cha soka cha Kuzu kilionekana kuvivutia klabu nyingi na kumsababishia asidumu kwenye klabu moja na kumfanya mismu mingi ya ligi kuhama hama ambapo mwaka 2015 mwanandinga huyo alihamia katika klabu ya Malindi na mwaka 2019 alichezea katika klabu ya Kilimani City.


Umuhimu wa Kuzu katika klabu mbali za soka ulionekana mpaka kwa uongozi wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) wakati huo ambapo alimchaguliwa kujiunga na kikosi cha timu ya taifa.
“Ndani ya kikosi cha taifa ‘Zanzibar Heroes’, nilidumu kwa miaka 12 mfululizo kuanzia mwaka 2001 mpaka 2013”, alisema.