Timu za Pemba zatoa msimamo
Zasema hazipo tayari kuvunja kanuni
NA ABDI SULEIMAN
VIONGOZI wa klabu zinazoshiriki ligi daraja la kwanza Taifa Pemba, wamesema hawana nia ya kugomea ligi, lakini hawako tayari kuwa sehemu ya uvunjaji wa kanuni mama ya mashindano kama ZFF inavyotaka kufanya hivi sasa.
Viongozi hao wamesema kanuni mama ya ZFF inaeleza kuwa ligi daraja la kwanza itachezwa kwa mizunguruko miwili, lakini hivi sasa ZFF inazishawishi klabu kumalizia ligi kwa mzunguruko mmoja, jambo ambalo ni uvunjifu wa kanuni ya mashindano.
Alisema kwa sasa kama ZFF wanataka kuendelea na ligi basi ichezwe kwa mizunguruko miwili kama ilivyoelezwa kwenye kanuni.
Msemaji wa klabu ambazo haziko tayari kuendelea na ligi Mohamed Khatib (Kishore), alisema klabu zimechoka kudharauliwa na viongozi wa ZFF kila siku, na sasa viongozi hao wanapaswa kukaa meza moja na viongozi wa klabu ili ligi iendelea.
“Rais na katibu wake wamekuja Pemba na kuondoka, huku wakishindwa kuonana na viongozi wa klabu, sasa wakati umefika kwa klabu kuonyesha umuhimu, kwani bila ya sisi hakuna mpira,”alisema.
Kishore alifahamisha kuwa klabu zinahitaji mpira uendelee, kwa maslahi ya kukuza soka la Zanzibar, huku akiishauri ZFF kupitia upya kanuni yao ya mashindano, ili klabu iweze kurudi uwanjani, ikizingatiwa mpira kwa sasa ni gharama kubwa.
“Tunashangaa kaimu katibu alikuja Pemba kukabidhi kombe la FA na kutoa agizo kwamba kutolewe ratiba michezo iliyobakia ichezwe, na ligi itakuwa imemalizika, haya mambo wapi yanatoka katika soka”alisema.