NA AMEIR KHALID

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, amesema sherehe za Tamasha la siku ya Kizimkazi (Kizimkazi day), iwe fursa ya kukuza uchumi na kuongeza mapato katika kijiji hicho.

Alitoa kauli hiyo huko Kizimkazi Mkunguni Wilaya Kusini Unguja, kwenye sherehe za tamasha la siku ya Kizimkazi (Kizimkazi Day), lililofanyika jana kijijini hapo.

Alisema umefika wakati sasa tamasha hilo liwe katika sura mpya ya kuinua uchumi wa kijiji, badala ya kuwa la sherehe za kawaida.

Katika hatua nyengine Samia alisema suala la ujenzi wa kiwanja cha watoto kijiji cha Kizimkazi Mkunguni, pia utachangia kwa kiasi kikubwa kuingiza kipato cha kijiji hicho.

‘’Wananchi wenzangu wa Kizimkazi asanteni sana kwa kujitokeza kwa wingi, na burudani mbalimbali mlizozitoa ili kuenzi mila, desturi na tamaduni zetu’’alisema.

Katika hatua nyingine Samia aliwashukuru wananchi wa Kizimkazi kwa kukubali ombi lao la kuanzishwa siku hiyo miaka 5 iliyopita, ili kuuenzi na kuutambulisha utamaduni wetu.

‘’Tumeweza kudumisha baadhi ya mila na desturi zetu na baadae kuendelea kuzirithisha kwa vizazi vyetu, ili kuhakikisha zinaendelezwa na kudumisha kizazi hadi kizazi’’alisema.

Pia aliwapongeza wazee wa Kizimkazi ambao kila mwaka wamekuwa wakijitokeza kwa wingi kuonyesha utamaduni wao, kwa vitendo au simulizi na wameweza kuwachukua vijana kwenye vikundi vyao.

‘’Wote tunajua muacha mila ni mtumwa hivyo basi niwasihi wazazi wenzangu, kuhakikisha hata ule utamaduni ambao hauonekani wala kusikika zinarithishwa kwa vijana wetu, ili nao waweze kuziendeleza na kuzirithisha’’alisema.

Aliongeza kuwa wote ni mashahidi maadhimisho ya siku ya Kizimkazi,yanaenda sambamba na uhamasishaji na ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo, jambo ambalo limekuwa sehemu ya utamaduni wao.

Alifafanua kuwa umefika wakati hivi sasa kuona namna gani wanaweza kuzifanya sherehe hizo ziwe kama sherehe za ZIFF ( Sauti ya busara ).

Pia alisema vyema kushirikiana na hoteli za kitalii katika ukanda huu kuleta wageni wao, kwenye sherehe hizo kwa kulipia ada kidogo,kutafuta wafadhili watakaoweza kutangaza biashara zao na kuitangaza siku hii.

Sherehezi hizo zimeasisiwa na Makamu huyo wa Rais na huu ni mwaka wa tano kufanyika, ambazo zilianza Agosti 7 kwa kutanguliwa na kisomo cha khitma kwa kuwarehemu wazee waliotangulia mbele ya haki, shughuli za usafi,michezo ya mipira pamoja na resi za ngalawa.