NA AMEIR KHALID
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, amewahimiza wananchi wa Zanzibar kutochagua viongozi wanaoendekeza rushwa ili wapigiwe kura.
Alitoa kauli hiyo huko Kizimkazi Mkunguni, wilaya Kusini Unguja wakati akizungumza na wananchi wa mkoa wa Kusini Unguja, kwenye tamasha la siku ya Kizimkazi (Kizimkazi Day), lililofanyika jana katika kijiji hicho.
Alisema ni wakati sasa wananchi kufahamu nani kiongozi bora ambaye ataweza kuwatumikia, hivyo ni vyema kuwaepuka na kutowachagua wale wote wanaotaka madaraka kwa kutoa rushwa.
Aidha aliwataka wagombea kufanya kampeni zinazozingatia sheria na kanuni za uchaguzi na wapiga kura kujiepusha na vitendo vya uvunjifu wa amani.
Akizungumzia kuhusu tamasha hilo, Makamu wa Rais ambaye pia ni muasisi wa tamasha hilo, aliwashukuru wananchi wa Kizimkazi kwa kuwa nae bega kwa bega na kukubali kwa moyo mmoja kupokea na kusimamia miradi ya maendeleo katika shehia, wilaya , mkoa na taifa kwa ujumla.
Alisema ni jambo la kujivunia kuona baadhi ya miradi imefanikiwa kupitia tamasha hilo tangu kuasisiwa kwake miaka mitano iliyopita na kutumika kwenye shughuli za kitaifa ikiwemo ukumbi wa mitihani skuli ya Sekondari Kizimkazi Mkunguni.
‘’Niseme kuwa miradi hii ya maendeleo sijafanya mwenyewe bali kwa msaada mkubwa wa wafadhili wetu marafiki zetu na ndugu zetu walio na mapenzi ya dhati kwa Wanakizimkazi, nao si wengine ni Ubalozi wa Japan, ‘SportPesa’, DSTV, NMB, NBC, CRDB, TFF, DATOGA na nyie wana Kizimkazi kwa kutoa maeneo na kusaidia kwenye shughuli mbali mbali za ujenzi,’’alisema.
Aidha alisema miradi yote isingezaa matunda iwapo wasingepata ushirikiano wa dhati kutoka kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.
“Nitoe rai kwenu kuitunza miradi hii ili itunufaishe zaidi kwa niaba ya wanakizimkazi, nasema ahsante sana niwaombe wafadhili wetu wote waendelee kutushika mkono, msituchoke,’’ aliongeza.
Alisema pamoja na mafanikio mengi yaliyopatikana anafahamu zipo changamoto, ambapo aliwahakikishia kushirikiana pamoja ili kuzipatia ufumbuzi unaofaa.
Alizitaja baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na kumalizia jengo la ofisi za SACCOS, uchakavu na ubovu wa majengo ya skuli ya msingi ukosefu wa ajira kwa vijana pamoja na kubuni fursa za kiuchumi.
Mapema Mkuu wa Mkoa Kusini Unguja Ayoub Mohammed Mahamoud alisema serikali ya mkoa tayari imekiweka kijiji cha Kizimkazi kuwa miongoni mwa vijiji, ambavyo vitawekwa taa za barabrani ili kuongeza uchumi wa kijiji hicho.
Tamasha la mwaka huu ni la tano toka kuasisiwa kwa lengo la kuimarisha mahusiano na kuchochea maendeleo ya shehia za Kizimkazi na mkoa wa Kusini Unguja ambapo shughuli mbali mbali hufanyika ikiwemo ya ujenzi wa miradi ya maendeleo.