NA MWANDISHI WETU, DODOMA

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Samia Suluhu Hassan, amewataka wanawake nchini kuacha tabia ya kutumika kusambaza umbea na majungu, badala yake washikamane ili wawe na maendeleo.

Samia aliyasema hayo wakati akifungua mkutano wa Baraza Kuu la Jumuiya ya Wanawake Tanzania (UWT), katika ukumbi wa Makao Makuu ya CCM Mjini Dodoma.

Alisema imekuwa ni jambo la kawaida katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu ndani na nje ya chama, wanawake wanatumiwa kusambaza umbea na majungu, jambo ambalo wanapaswa kuliacha.

Alisema ikiwa wanawake watashikamana upo uwezekano mkubwa wa kuwa na maendeleo ya haraka yatayowafanya kuinua hali zao za kiuchumi na kukijenga vyema Chama cha Mapinduzi.

“Na hapa nataka kupiga mstari ndimi zetu, tukizitumia ndimi zetu vizuri, basi mambo yatakuwa mazuri, kwa sababu wanawake ni wazuri wa kutoa habari, lakini kwa bahati mbaya tunatumia ndimi zetu kueleza mabaya zaidi”, alisema Samia.

Samia ambaye ni mjumbe wa kamati kuu ya CCM taifa, alisema inasikitisha ndani ya Jumuiya ya Wanawake kumekuwa na wanachama wanaotumika kuwaangusha wanawake wenzao, jambo ambalo halileti picha nzuri.

Alisema kumekuwa na kawaida katika kila jambo baya linalopangwa, wanawake wanatumika kufanya vitu ambavyo vinawaresha nyuma wanawake wenzao, jambo ambalo lihajitaji kuacha tabia hiyo.

Alisema kuwa wanawake wanapaswa kutambua kwamba jukumu la kulainisha mitambo ya uchaguzi kwa upande wa Chama cha Mapinduzi (CCM) limekabidhiwa kwa Jumuiya hiyo UWT na hawapaswi kuwa chanzo cha kukikosesha ushindi chama hicho.

Alisema kampeni ni jukumu zito na wanahitaji kujipanga ili kuhakikisha Chama cha Mapinduzi kinashinda katika uchaguzi huo, hasa ikizingatiwa kuwa tayari chama kimesimamisha wagombea wazuri.