BADO tunaamini kilimo katika visiwa vya Zanzibar ndio uti wa mgongo wa uchumi wa nchi yetu hasa ikizingatiwa kuwa bidhaa zinazouzwa nje ndizo zinazoingiza fedha nyingi za kigeni.

Miongo kadhaa sasa Zanzibar imekuwa ikilitegemea zao la karafuu kama zao kuu la kibiashara linalozuzwa nje ya nchi, lakini mwishoni mwa miaka ya 1980 zao hilo liliporomoka bei katika soko la dunia.

Hata hivyo nchi haikukata tamaa kwani pamoja na kuanguka kwa bei katika soko la dunia, katika miaka ya karibuni zao la mwani nalo limejumuishwa kwenye orodha ya mazao yanayouzwa nje.

Pamoja na uzalishaji wa mazao ya biashara, wakulima wa Zanzibar pia ni wakulima wazuri wa mazao ya chakula na matunda kwa ajili ya matumizi ya kila ya maisha ya wananchi.

Pamoja na sekta ya kilimo kukabiliwa na changamoto nyingi, serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejitahidi katika kuzipatia ufumbuzi changamoto za wakulima.

Kwa mfano serikali imeshusha bei za pembejeo za kilimo dawa za kuulia magugu, dawa za kuulia wadudu, mbolea na kadhalika kwa asilimia 75, ambapo mkulima anagharamia asilimia 25 iliyobakia.

Hivi karibuni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein alifungua maonesho ya tatu ya kilimo ambayo hufanyika kila mwaka katika viwanja vya Dole.

Katika mengi aliyozungumzia wakati wa ufunguzi wa maonesho hayo, Dk. Shein alieleza jinsi serikali ilivyobuni na kutekeleza mikakati ya kuimarisha kilimo visiwani Zanzibar.

Kwa hakika mipango na mikakati yote ya kilimo iliyobuniwa na kutekelezwa na serikali, ililenga kuhakikisha Zanzibar inakuwa na uhakika, usalama wa kuwa na chakula na lishe kwa wananchi wote.

Hata hivyo unapotembelea mabanda ya maonesho ya biashara na kuangalia namna taasisi za umma na binafasi zinavyoendesha shughuli za kilimo ikiwemo mifugo unaona hasa mafanikio makubwa yaliyopatikana.

Kwenye maonesho hayo unaona hasa utaalamu wa kilimo, mifugo na uvuvi unavyo fanyiwakazi na kuleta tija, ambapo kama wakulima wa kawaida wakishirikishwa na kuwezesha kupewa utaalamu bila shaka Zanzibar ingejitosheleza kwa chakula.

Hata hivyo, chakusikitisha ni kwamba wakulima, wafugaji na wavuvi wa kawaida hawajawa na uwezo mkubwa wa kitaalamu na kiuwezeshwaji kiasi kwamba wanatumia nguvu nyingi kuliko tija kwenye mavuno.