Dk. Shein asema SMZ inaimarisha hatua kwa hatua

NA MWANAJUMA MMANGA

LEO ni kilele cha siku ya kilimo duniani ambapo siku hii huadhimishwa kila ifikapo Agosti 8 ya kila mwaka dunia kote.

Pamoja na mambo mengine lakini Siku hiyo ina lengo la kutambua umuhimu wa sekta ya kilimo, hasa kwa Tanzania ambapo miaka mingi tumezoea kuita kilimo kuwa ni uti wa mgongo wa uchumi wa nchi.

Hata hivyo, Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kila ifikapo Agosti mosi ya kila mwaka serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Kilimo, Maliasili Mifugo na Uvuvi inafanya maonesho ya kilimo takriban miaka mitatu sasa ili kuonesha bidhaa zinazotokana na sekta ya kilimo.

Mwaka juzi maonesho hayo yalifanyika Pemba katika kijiji cha Chamanangwe na mwaka jana kufanyika huko Dole Unguja ambapo kiujumla wake maonesho hayo yalitoa hamasa kubwa kwa wakulima, wafugaji na wajasiriamali ambapo wananchi walipata mwamko wa kulima kilimo cha mazao mbali mbali ya biashara na chakula.

Kwa mwaka huu Maonesho ya kilimo yamefunguliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein huko Kizimbani Wilaya ya Magharib ‘A’ Unguja.

Rais Shein alisema serikali kwa kuzingatia umuhimu wa chakula na lishe serikali inaendelea kutekeleza kwa vitendo sheria namba 5 ya mwaka 2011, ambayo inatoa uhakika wa kuwepo kwa chakula nchini.

Dk. Shein alisema sheria hiyo ni kuandaa mazingira yatakayoiwezesha Zanzibar kwa wakati wote kuwa na chakula cha kutosha, lishe iliyokuwa bora.

Alisema, mikakati mengine ni mpango wa maendeleo wa miaka 10 wa sekta ya kilimo, mpango wa maendeleo ya uvuvi na mkakati wa mazao ya baharini.

Dk. Shein alibainisha kwamba mikakati hiyo imelenga kuongeza uzalishaji kwa kutumia mbinu bora, teknolojia za kisasa, ujenzi wa miundombinu, upatikanaji wa masoko, upatikanaji wa mitaji na uhifadhi wa chakula ili kuongeza tija, kipato, kuondoa umasikini na kukuza uchumi wa nchi.

Alisema kati ka kuimarisha sekta hiyo kwa mwaka wa fedha 2020/2021 serikali imeongeza bajeti kutoka shilingi bilioni 88.17 hadi 2019/2020 hadi kufi kia bilioni 129.89 kwa mwaka 2020/2021 ambapo ongezeko hilo ni sawa na asilimia 47.3.    

Alibainisha kuwa maonesho hayo yamebuniwa kwa makusudi na mambo mbalimbali ikiwemo kuwa na hamasa wananchi kutumia vizuri rasilimali ya ardhi kati ka shughuli zenye faida kwao kwa lengo la kupata tija ya kupitia sekta hiyo.

Alisema jambo jengine ni kuwashajihisha wakulima kuongeza bidii katika kuimarisha bidhaa ili ziweze kuwa na ubora unaohitajika sambamba na kuwajumuisha na kuwashajihisha wananchi ili wapate fursa ya utaalamu na njia ya kuimarisha ubora wa bidhaa.

Alifahamisha kuwa kuwepo kwa maonesho hayo ni fursa muhimu kwa wananchi kupata taaluma, kujitangaza, kutoa ajira na kuunganishwa na masoko kwa lengo la ukuaji wa sekta ya kilimo na ukuaji wa uchumi wa nchi na kwa ujumla.

Aidha alisema sekta ya kilimo ni sekta mama ambayo imegusa mambo mbali mbali ikiwemo sekta ya utalii ambayo inachangia pato la taifa kwa asimilia 27 kupitia viungo.

Sekta ya kilimo imekuwa ikitoa mchango wa moja kwa moja kwa wananchi katika kujikimu kimaisha ambapo asilimia 40 wameajiriwa na sekta hiyo na inakadiriwa kuwa zaidi ya asilimia 70 ya wananchi wanategemea sekta hiyo ambayo imeongoza kwa ukuaji katika Pato la Taifa.

Kwa upande wake Kaimu Waziri wa Wizara ya Kilimo Maliasili Mifungo na Uvuvi, Haji Omar Kheir, alipongeza hatua ya serikali ya awamu ya saba kwa kuiendeleza sekta ya kilimo.

Aliahidi wizara itaendeleza maonesho hayo ili kuona wakulima wanapata fursa ya kutangaza na kuimarisha kilimo chao kwa maslahi yao na taifa kwa ujumla.   

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Maryam Juma Sadala, alisema maonesho hayo yamejumuisha taasisi 219 kwa mwaka huu ukilinganisha na mwaka jana walikuwa 172 ambayo ni hatua maendeleo makubwa ambayo yameonesha ari na muamko kwa wadau mbalimbali wa sekta hiyo.

Hata hivyo, alisema wamefanya jambo la busara kuanzisha maonesho hayo ambayo yanawaunganisha wakulima, wafugaji wavuvi na wahifadhi mazingira katika kutoa huduma na kupata fursa ya kuona maendeleo ya sekta hiyo hapa nchini.

Alisema maonesho hayo yanaunganisha watu mbalimbali kwa kutoa huduma na kuunganisha fursa zilizokuwepo ili waweze kupiga hatua katika kupambana na umasikini na kupiga hatua katika uchumi wa nchi.

Maonesho hayo yamegharimu zaidi ya shilingi milioni 71 ambazo zinatoka serikalini na zaidi ya shilingi milioni 12 zimechangiwa na washiriki na wajasiriamali ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ya nane nane ni ‘Tudumishe amani na utulivu kwa maendeleo ya sekta ya kilimo Zanzibar.