NA MADINA ISSA

NAIBU Waziri wa Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati, Juma Makungu Juma, amesema uzinduzi wa sera ya taifa ya ardhi ya Zanzibar, utasaidia kuondosha changamoto kadhaa zinazoikabili sekta hiyo kwa wakati huu.

Naibu huyo alieleza hayo katika hafla ya uzinduzi wa sera hiyo, iliyofanyika katika ukumbi wa Dk. Ali Mohamed Shein uliopo katika jengo la Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (ZURA).

Alisema, sera hiyo itasaidia kuongoza utawala na matumizi bora ya ardhi iliyokuwepo na rasilimali zake kwa kuhakikisha inatumiwa na kusimamiwa katika namna bora na endelevu zaidi kwa manufaa ya wananchi.

Alisema utekelezaji sahihi wa sera hiyo unahitaji mashirikiano ya wadau mbalimbali ikiwemo wanaohusika moja kwa moja na shughuli za uendeshaji wa ardhi.

Makungu alisema ana imani kwamba wizara na wadau watashiriki kwa kuchukua hatua zinazostahiki katika kuyafahamu majukumu na dhamana zao na kuitekeleza vyema sera hiyo, hali ambayo itasaidia matumizi sahihi na endelevu ya ardhi.

Aidha alisema kuwa sera hiyo pia itaongoza haki ya kumiliki au kufikia kumiliki, katika kuelekeza matumizi na usimamizi wa ardhi kwa ajili ya kuleta maendeleo ya kijamii, kiuchumi, kisiasa na kimazingira kuelekea lengo la kuondoa umaskini.

“Natambua jitihada za kila mmoja ikiwemo wafanyakazi wa wizara ya Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati na Kamisheni ya Ardhi kwa juhudi kubwa mlizozifanya za kutayarisha sera”, alisema.

Hata hivyo, Naibu huyo, aliwapongeza wadau walioshiriki katika kukamilika kwa utayarishaji wa sera hiyo wakiwemo viongozi na wajumbe wa taasisi za serikali na zisizo za serikali kwa mashirikiano na michango yao.

Sambamba na hayo, aliwashukuru washirika wa maendeleo katika mradi wa usimamizi endelevu wa ardhi na mazingira (SMOLE II) kwa msaada wao uliowezesha ukusanyaji wa maoni ya wananchi ambayo ilikua ndio msingi wa utayarishaji wa sera hiyo.