NA MARYAM HASSAN

JAMII inashauriwa kujenga utamaduni wa kuzitumia Maktaba zilizopo nchini kwa lengo la kujiongezea maarifa, kwani inaonekana bado mwamko ni mdogo kwa wanaozitumia huduma hizo.

Wito huo umetolewa na Mwanachama wa Shirika la Huduma za Maktaba, ambayeni mwanafunzi wa skuli ya Hamamni, Samir Abdalla Makame, wakati akizungumza na Zanzibar Leo huko katika ofisi zake Maisara Mjini Unguja.

Alisema wanafunzi wengi wamekuwa wakishindwa kutumia huduma za shirika hilo kutokana na bado hawalifahamu wapi lipo, jambo ambalo huwajenga kutokuwa na utamaduni wa kujisomea.

Alisema hiyo ni kutokana na kuwa skuli nyingi za serikali hazina vitabu vya kutosha kutokana na wingi wa wanafunzi ambao wanahitaji huduma hizo.

“Nitoe mfano wakati nasoma katika skuli ya Hamamni kipo kitabu kimoja tu cha Human Geografi kwenye maktaba ya skuli huku idadi ya wanafunzi wanaokihitaji kitabu hicho ni zaidi ya 100, lakini alisema alipofika katika Shirika la Maktaba vitabu hivyo vipo vingi na vyakutosheleza” alisema Samir.