NA MWANAJUMA MMANGA

SERIKALI imesema itaendelea kuwaunga mkono vijana kutokana na jitihada zilizochukuliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein ili kufanikisha malengo yao katika kujiletea maendeleo.

Naibu waziri wa Biashara na Viwanda, Hassan Khamis Hafidh alieleza hayo jana kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Baraza la Mapinduzi na Kiongozi, Dk. Abdulhamid Yahya Mzee kwenye maadhimisho ya siku ya vijana iliyofanyika huko katika kiwanja cha kufurahishia watoto kariakoo mjini Zanzibar.

Alisema vijana ndio rasilimali ya taifa, hivyo serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itakuwa pamoja nao katika kuhakikisha wanafanikisha katika malengo yao ya kujiletea maendeleo.

Alisema serikali ya awamu chini ya uongozi wa Dk. Ali Mohamed Shein imewawezesha vijana katika nyanja mbali mbali kwa lengo la kuwakwamua na uamsikini na kupanga hatima ya maisha yao.

Alisema nyanja hizo ni pamoja na elimu, ajira na ujasiriamali ambao huwawezesha vijana kujiajiri wenyewe na kutosubiri ajira ya serikali kwani kumekuwa na ongezeko kubwa la vijana hapa nchini.

Hivyo aliwataka vijana hao kufuata miongozo na sheria zilizopo za kufuata taratibu za serikali kutojiingiza katika vitendo vibaya vya matumizi ya madawa ya klevya na uvunjifu wa mania nchini.

Aidha aliwataka kujiepusha na vitendo vya uvunjifu wa amani katika kipindi cha uchaguzi mkuu ujao na takae fanya hivyo atachukuwa sheria dhidi yao.

“Serikali imejipanga kuwachukulia hatua za nidhamu wale wote watakaojihusisha na vitendo vya uvunjifu wa amani katika uchaguzi mkuu ujao hivyo mhakikishe mnaweka amani na utulivu”, aliongeza kusema.

Pia aliwashukuru vijana waliojitokeza katika uchaguzi wa nafasi mbali mbali majimboni ambao inaonekana wapo baadhi yao walifanikiwa kuingia katika awamu ya pili katika uchaguzi wa wabunge, uwakilishi na madiwani.

Nae Naibu Katibu wa Wizara ya Uijana, Utamaduni Sanaa na Michezo, Amour Hamil Bakari,  aliwataka vijana kushiriki kikamilifu katika kipindi cha uchaguzi mkuu kwa njia ya amani na utulivu.

Alisema vijana mara nyingi huwa wanashirikishwa katika masula ya uvunjifu wa amani na wanasiasa hivyo ni vyema kutokubali shirikishwa kwani inaweza kutoweka kwa amani katika nchi.

Aidha alisema siku ya vijana ina lengo la kuwahamasisha kushiriki kikamilifu kwa njia ya amani na utulivu katika hatua zote za uchaguzi, kampeni na baada ya uchaguzi mkuu pamoja na matokeo ya uchaguzi mkuu wa ngazi mbali mbali kudumisha amani.

Kwa upande wake ofisa Uhusiano wa benki ya damu salama Zanzibar Bakari Omar Magarawa aliwataka vijana kuchangia damu ili kuokoa maisha ya mama wajawazito na wanaopata ajali.

Alisema matumizi ya damu kwa siku ni chupa 75 lakini hivi sasa kumekuwa na uhaba wa damu tangu kipindi cha Corona.

Maadhimisho hayo yameadhimishwa kwa uchangiaji wa damu na jumla ya chupa 55 zilizopatiokana ambapo ujumbe wa mwaka huu “Kijana shiriki uchaguzi  dumisha amani”.