NA ZAINAB ATUPAE
NAIBU Waziri wa Vijana,Utamaduni,Sanaa na Michezo Zanzibar Lulu Msham Abdalla,amesema wataendelea kutekeleza agizo la Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein, la kuwatembelea wasanii wa zamani na wagonjwa kwa lengo la kuwafariji.

Lulu aliyasema hayo wakati wa ziara ya kuwatembelea na kuwafariji wasanii wagonjwa na wazee kwa upande wa Unguja.
Alisema Serikali inathamini sana mchango na nguvu za wasanii hao, ambazo walizitoa wakati wa ujana wao, hivyo wataendelea kukumbukwa kutokana na mchango wao huo.
Hata hivyo alisema ingawa ziara hiyo ni mwanzo lakini wataendelea na itakuwa endelevu, ili kuwapa moyo na kujihisi kuwa na wao ni sehemu ya jamii.

Aidha Naibu huyo aliwataka wasanii hao kutambua kuwa Serikali inakumbuka sana michango yao walioitoa enzi zao kwa kuelimisha jamii kupitia Sanaa walizokuwa wakifanya.
Lulu aliwambia wasanii hao kuwa wataendelea kutafuta vijana ili kuwahamasisha kujiunga na sanaa,ikiwemo nyimbo na maigizo ili kupata vijana watakaoitangaza nchi yao kupitia Sanaa zao.

Katibu Mtendaji Baraza la Sanaa, Sensa, Filamu na Utamaduni ambae pia ni Kaimu Kamishna Idara ya Utamaduni na Sanaa Zanzibar Dk. Omar Abdalla Adam, aliwashukuru wasanii hao kwa mashirikiano wakati wa ziara hiyo.

Alisema walipanga kuwatembelea wasanii 28 Unguja 20 na Pemba wanane, lakini kutokana na hali wamelazimika kuwatembelea wasanii 21 Unguja 11 na Pemba 10.
Aidha alifahamisha kuwa zoezi hilo ni muendelezo wa maadhimisho ya shamra shamra za

Tamasha la 25 la Utamaduni wa Mzanzibari.
Fatma Issa Juma msanii wa zamani wa taarabu aliwashukuru viongozi hao kwa juhudi walizozifanya,huku akiwataka kuendelea kuwatembelea kila baada ya muda, kwani wanafarajika sana kuona Serikali bado inakumbuka michango yao.

Wasanii waliotembelewa jana ni Fatma Issa Juma, Mwapombe Hiyari, Fatma Haji Mlenge, Jaza Hamad ‘Betele’,Nihifadhi Abdalla, Sihaba Juma, Aziza Abdalla na Kassim Ali Nassor.