NA HAFSA GOLO
WAKAAZI wa Shehia ya Jang’ombe Urusi, wametakiwa kuhakikisha wanatunza stahiki zao za kupigia kura, ili waweze kutumia haki yao ya demokrasia ya kuchagua viongozi katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.
Sheha wa shehia hiyo,Yussuf Haji Mtumwa, alieleza hayo wakati alipokua akizungumza na wanachi wa shehia hiyo juu ya umuhimu wa kutunza shahada hizo na kushiriki katika uchaguzi mkuu kikao kilichofanyika huko Jang’ombe mjini Unguja.
Alisema ni vyema wananchi hao kutokubali kurubuniwa na baadhi ya wanasiasa ambao hawana mitazamo sahihi yenye kuzingatia maslahi mapana ya nchi na hatimae wakapoteza kutumia fursa ya kuchagua viongozi.
Aidha alisema jambo muhimu la kuzingatiwa katika kipindi kinachoelekea uchaguzi mkuu ni pamoja na kudumisha amani na utulivu, sambamba na kujiepusha katika vitendo vinavyochangia kuleta mizozo miongoni mwao ama hamasa zitazochangia ukiukwaji wa sheria za nchi.
Aliwambia wakaazi wa shehia hiyo, kuhakikisha wanatii na kufuata sheria za uchaguzi na taratibu za nchi ikiwa ni pamoja na suala zima la kuepuka siasa za fujo na vurugu kuanzia kampeni hadi uchaguzi mkuu.
“Hatutomvumilia mtu yoyote atakaebainika kwenda kinyume na matakwa ya nchi, ikiwemo kuvuruga amani kwa kisingizio cha uchaguzi “,alisema.
Mbali na hilo, aliwataka vijana kushirikiana kwa pamoja katika kuhamasishana juu ya umuhimu wa kuheshimu sheria na kudumisha Amani, iliyopo hasa ikizingatiwa wanawake ni miongoni mwa watu watakaoathirika zaidi.