Fahamu umuhimu wa tembo kijami, kiuchumi na kiutamaduni

NA MWANDISHI WETU

JANA Dunia iliadhimisha siku ya tembo duniani, siku hii ni makhsusi kwa ajili ya kuwalinda, kuwaenzi na kuwahifadhi wanyama hao wanaoonekana kutoweka kwa kasi kutokana na kuwindwa ili watu kupata pembe zao.

Katika makala haya maalumu tunazungumzia umuhimu wa mnyama tembo katika maisha yao ya kila siku na mazingira aliyonayo.

Tembo ni mnyama wa nchi kavu jamii ya mamalia. Ndiye mnyama mkubwa kuliko wote waishio nchi kavu na Kuna aina mbili za tembo duniani.

Tembo wa bara la Afrika na tembo wa bara la Asia, kuna spishi mbili za tembo wa Afrika, nao ni embo wa msituni na tembo wa uoto wa savana.

Tanzania ina tembo wa savana pekee, ambapo Tembo wa msituni hupatikana katika nchi za Afrika ya Kati na Magharibi.

Tembo anakadiriwa kuwa na uzito wa kilo 6600 (tani 6.6) kwa madume na kilo 3300 (tani 3.3) kwa majike. Tembo huishi miaka 60 hadi 70 na hupendelea kula mimea, magome ya miti, matunda,majani na nyasi.

Kuna tofauti kati ya tembo dume na tembo jike ambapo tembo dume huwa na mwili mkubwa uliojengeka, paji la uso huwa na mviringo lakini tembo jike huwa na paji lililochongoka.

FAIDA ZA TEMBO KIUCHUMI

Hapa nchini, kwa zaidi ya asilimia 90 ya utalii unategemea wanyamapori ambapo watalii wengi huja kuwaona wanyama, kuwapiga picha na kuondoka.

Wanyamapori hawa wamebeba utalii kwa kiasi kikubwa na utalii umesaidia kukuza uchumi wa nchi hii.

Aidha wanyama hawa kupitia utalii wanasaidia kupata fedha za dawa, vitabu maskulini na wanatujengea barabarana miundo mbinu nyingine na pia wanalipa mishahara kwa watumishi wa umma.

HUCHANGIA PATIKA PATO LA TAIFA

Tembo pamoja na wanyamapori wengine wamekua kivutio kikubwa cha utalii hivyo hutusaidia kupata hata fedha za kigeni ambazo husaidia maendeleo ya kiuchumi ya nchi yetu. Mfano sekta ya utalii kwa mwaka 2016 ilichangia asilimia 17.5 ya pato la taifa na asilimia 25 ya fedha za kigeni.

CHANZO CHA AJIRA

Uwepo wa tembo na wanyama wengine umepelekea watu wengi kuajiriwa katika sekta ya wanyamapori na utalii. Kwa mfano mwaka 2016, watu takriban 600,000 waliajiriwa moja kwa moja katika sekta ya utalii na wengine takriban milioni 1 katika ajira mbadala.

NI KIVUTIO CHA WATALII

Tembo ni mnyama ambaye ana mvuto sana kutokana na ukubwa, uzuri wake wa asili na muundo wa jamii na tabia yake. Takwimu za mwaka 2016 zinaonyesha kuwa watalii waliotembelea Tanzania walikua 1.284,279 ambao ni ongezeko la asilimia 12.9 ukilinganisha na mwaka 2015 ambao watalii waliofika Tanzania walikua milioni 1,137,182.

FAIDA ZA TEMBO KITAMADUNI

Tembo ni urithi wa Taifa letu, ambapo mnyama huyu ana umuhimu sana katika utamaduni wa kiafrika.

Kwa mfano, hutokea katika mapambo kama vile hereni, pete na hata michoro ya kwenye mavazi.

Aidha tembo wana nafasi maalumu katika hadithi za kiafrika, hivyo wanyama hawa kama wanyama wengine ni urithi wa taifa letu.

FAIDA ZA TEMBO KIMAZINGIRA.

Tembo ni mnyama tegemeo kwa wanyama wengine na muhimili mkubwa katika mfumo wa ikolojia.

Mfano, wakati wa kiangazi tembo hutumia meno yao kuchimba maji ardhini, hii huwawezesha tembo kuishi katika mazingira kame.

Maji hayo huwafaidisha wanyama wengine wakubwa na wadogo na pia wakati wa kiangazi tembo huangusha matawi makubwa ya miti ambayo huwawezesha wanyama wadogo kupata chakula mfano swala, pundamilia na hebivora wengine.

Sambamba na hilo, tembo husaidia kusafisha na kutengeneza mazingira ya mbuga. Tembo wasingekuepo, mazingira ya savana yangeonekana tofauti sana na hasa kutokana na kula mimea na vichaka vya miti ambapo hufungua misitu na mapori kuwa mbuga wazi kutoa nafasi kwa mimea mengine kuota na njia kwa wanyama wengine.

Aidha wanyama tembo husaidia kuongezeka kwa idadi ya mimea na hii ni kutokana na ulaji wao wa mimea yenye mchanganyiko wa mbegu mbalimbali.

Popote wanapoishi huacha kinyesi kilichojaa mbegu, ambapo mbegu hizi huchipua na kuwa nyasi, miti na hata misitu hivyo husaidia kuongezeka kwa mimea na afya ya mazingira kwa ujumla.

Kinyesi cha tembo ni chanzo cha chakula kwa wanyama kama tumbili, ndege na nyani. Pia kuna wadudu hutegemea kinyesi cha tembo kama chakula mfano mende kibyongo (dung beetle). Kinyesi cha tembo pia ni chanzo cha rutuba katika udongo hivyo kuongeza afya ya mazingira.

CHANGAMOTO ZINAZOWAKABILI TEMBO

Pamoja na faida nyingi za tembo, kuna changamoto nyingi zinazomkabili mnyama huyu mfano ujangili na migogoro baina yao na binadamu.

Ujangili umeongezeka kutokana na uwepo wa biashara ya meno ya tembo katika masoko ya bara la Asia.

Hivyo, Serikali inapaswa kuunga mkono jitihada za kimataifa za kuikakabili biashara hii kwani kuna mataifa tayari wameshaonyesha nia ya kufunga masoko kwa mfano China.

Jukumu la kuzuia ujangili si la serikali pekee, dhana hii ni potofu kabisa kwani, uzuiaji ujangili kamwe hautafanikiwa kama wananchi na wadau wengine walioko ndani na nje ya nchi yetu wataendelea kubakia watazamaji tu.

Ni muhimu kila mwananchi mzalendo wa nchi hii ashiriki kikamilifu katika ulinzi wa nchi na rasilimali zake zote kama katiba ya nchi inavyotuasa.

Elimu kuhusu dhoroba za tembo na mienendo ya tembo inafaa kutolewa kwa watu waishio pembezoni mwa maeneo ya hifadhi.  Hii itapunguza shughuli za binadamu katika maeneo hayo hivyo kuepusha migogoro hii.     

Wanyamapori, tembo wakiwemo kama ilivyo kwa viumbe hai, huzaliana na hivyo, kama tutashirikiana kuwalinda na kuwatumia kiendelevu si miaka mingi tangu sasa watakuwa namba moja katika kuchangia pato la Taifa letu.