LONDON, England
MANCHESTER City imeandaa ofa ya pauni milioni 89.5 pamoja na wachezaji watatu, Bernardo Silva, Gabriel Jesus na Eric Garcia kwa Barcelona ili kumsajili mshambuliaji wao hatari, Lionel Messi.

Matajiri wa ManCity wana matumaini ya kufikia makubaliano na miamba hiyo ya Catalanya baada ya Messi mwenyewe kutangaza kutaka kuondoka Nou Camp msimu huu.
Endapo Messi atakubaliana na ManCity, atakwenda kuungana na kocha wake wa zamani, Pep Guardiola ambaye kupitia yeye alikuwa na mafanikio makubwa kwenye kusakata soka Barcelona akifunga jumla ya magoli 634, na usaidizi 285 katika mechi 731 alizocheza.

Wawili hao wanadaiwa kuwa na mawasiliano kupitia njia ya simu kuhusu kujiunga na Etihad, hata pia mazungumzo ya jinsi gani Messi ataweza kuishi England na kujifunza lugha ya Kiingereza baada ya kuishi Hispania kwa miaka 20.

Wazo la ManCity kumsaini Messi linaonekana ilikuwa ndoto za muda mrefu, lakini, kwa dau hill la pauni milioni 89.5 likiwa pamoja na wachezaji Silva, Jesus na Garcia linaweza kutimiza malengo yao ya usajili.

Kwa mujibu wa Sport, mawasiliano yamefanywa na kiongozi wa Barca kumleta, Jesus hapo Nou Camp. Jesus amekuwa ni mlengwa namba moja kwa Barcelona ili kuchukua nafasi ya Luis Suarez.

Messi amekuwa akisema kwa sasa ni mchezaji huru na anaweza kuondoka na anaweza kwenda kujiunga na klabu yoyote.

Lakini, hilo ni tofauti na Barcelona ambayo wanadai bado ana mwaka mmoja na akiwa na akiwa na kifungu cha kutolewa kwa pauni milioni 629.

Iwapo ManCity itaamini maneno hayo ya Messi ni sahihi kuwa yupo huru, italazimika kupata (ITC) kutoka Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) na kumsajili ili kuanza kuwatumikia msimu wa 2020/21 utakaoanza mwezi Septemba.

FIFA ndiyo yenye uwezo wa kuamua mzozo utakaojitokeza kati ya Barcelona na Manchester City inayotaka kumsajili Messi kwa ajili ya msimu ujao.

Endapo, FIFA, itasema Messi yupo sahihi kuwa ni mchezaji huru, moja kwa moja atajiunga na ManCity, lakini, kama FIFA itasema Barcelona ndiyo ipo sahihi, ManCityitalazimika kutoa kitita hicho cha fedha kama inamuhitaji.

Mkataba wa mwisho Messi aliyoanguka saini mwaka 2017 ulimpa ruksa ya kuondoka bure kila ifikapo mwisho wa msimu kama atahitaji kufanya hivyo na kutoa taarifa mapema katika siku 10 za kwanza za mwezi Juni.

Lakini endapo hakutakuwa na taarifa zozote kutoka kwa Messi za kuomba kuondoka baada ya kupita siku 10 za mwanzo za mwezi Juni, klabu itachukulia kuwa dirisha hilo limepita kwa maana hiyo atakuwa na mwaka mwengine ndani ya timu.

Messi anatafsiri tofauti, kama mkataba unamruhusu kuondoka kama mchezaji huru kila mwishoni wa msimu, na msimu huu haukuisha hadi mwezi Agosti, hivyo, anaamini anaweza kwenda pasipo malipo.(Goal).