NA MWANDISHI WETU

LEO Jumapili, wapenda soka Tanzania bara watashuhudia mchezo wa mwisho kwa msimu huu wa soka wa 2019/20 Tanzania Bara, ambao ulianza mwezi Agosti, 2019.

Mchezo huo wa kufunga msimu huu utakuwa ni wa fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam maarufu Kombe la FA utakaozikutanisha Namungo FC dhidi ya Simba SC.

Mchezo huo utapigwa uwanja wa Nelson Mandela Sumbawanga mkoani Rukwa.

Kila upande umekuwa ukijinasibu kuibuka na ushindi, Simba wamepania kushinda huku wakitaka kuchukua taji la tatu msimu huu, Namungo wao wanataka kuchukua taji hilo na kuweka heshima.

Namungo msimu huu ni wa kwanza kucheza Ligi Kuu Bara, pamoja na kushiriki mashindano hayo, wamefanya vizuri katika ligi na kumaliza nafasi ya nne ikiwa na pointi 64. Simba ni mabingwa wakikusanya pointi 88,timu zote zilicheza mechi 38.

Katika ligi, timu hizo zimekutana mara mbili, Simba imeibuka wababe kwa kushinda mechi moja na sare moja, hivyo Namungo wana muda wa kujiuliza.

Mchezo ni mmoja kati ya mchezo ambao utakuwa wa kuvutia sana kutokana na timu zinazokwenda kukutana.

Kitendo cha Namungo kupanda daraja na kumaliza ndani ya nne bora kwenye ligi si cha kubeza. Hii inakumbusha KMC ya msimu wa 2018/19 ambayo ilikwenda kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika.

Kocha Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck amesema kuwa licha ya maandalizi waliyokuwa nayo kwa siku kadhaa, lakini anaona uwanja wa Nelson Mandela unaweza kumharibia.

Kocha huyo ameongeza kuwa, licha ya yote hayo lakini bado hesabu zake zote ni kuhakikisha kwamba ubingwa wa kombe hilo anautia mkononi.

Sven raia wa Ubelgiji amesema uwanja huo unaweza kuwa kikwazo kwao kutokana na kutokuwa sawa kwa asilimia 100 lakini hawana namna zaidi ya kupambana na wapinzani wao.

“Hii ni mechi muhimu kwetu na tumekuwa na maandalizi nayo kwa kipindi kirefu, tukianzia na zile mechi mbili za mwisho za ligi kabla ya kwenda Mbeya.

“Itakuwa ngumu na tunatakiwa kujiweka sawa zaidi kuliko wapinzani kwa sababu ya wapinzani wetu walivyo lakini pia aina ya uwanja ambao tutauchezea.

“Uwanja siyo mzuri sana lakini hakuna namna zaidi ya kupambana kwa sababu, lengo letu tunalolitaka ni kuona tunashinda ubingwa huu kama ambavyo tumekuwa tukitamani kuona tunafanikisha hilo,” alimaliza Sven.

Simba ilitinga hatua ya fainali kwa ushindi wa mabao 4-1 mbele ya Yanga huku Namungo FC ikishinda kwa bao 1-0 mbele ya Sahare All Stars.