NA ASIA MWALIM

JESHI la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja limewakamata  watu sita kwa tuhuma ya wizi wa mifugo Ng’ombe.

Kamanda wa Polisi Mkoa huo ACP, Awadh Juma Haji hayo akitoa taarifa za matukio ya wiki katika Mkoa huo, huko ofisini kwake Mwembe Madema Mjini Zanzibar.

Kamanda Awadh alisema operesheni iliyofanywa na Jeshi hilo katika kipindi cha sherehe za Skukuu ya Eid el Hajj wamefanikiwa kiasi kikubwa kupambana na kuwakamata watuhumiwa hao.

Alisema katika opereshen hiyo walifanikiwa kukamata watuhumiwa sita ambao ni Ali Salum Ramadhan (45) mkaazi wa Kombeni, Twalib Juma Khamis (32) mkaazi wa Mungani, Juma Mwita Juma (43) mkaazi wa Amani, Mohammed Amour Ali (59) Kisakasaka, Zakaria Charles (25) mkaazi wa Kisakasaka Juma Sharif Masoud (44) mkaazi wa Kombeni.

Kamanda huyo alisema watuhumiwa waliiba ng’ombe sita wenye rangi tofauti wenye thamani ya shilingi milioni tano na laki moja ambao walikua wamehifadhiwa kwaajili ya kuchinjwa na kutolewa sadaka kwa wananchi.

Alifahamisha kuwa ng’ombe hao ni mali ya Jumuiya ya Kiislamu ya Uturuki, ambayo inajishughulisha na utoaji sadaka kwa baadhi ya wananchi katika kipindi cha sherehe za skukuu.

Kamanda Awadhi alisema Ng’ombe hao waliibiwa Agosti 1 ,mwaka huu majira ya saa 2:00 asubuhi wakiwa wamehifadhiwa machinjioni kwenye zizi huko Kisakasaka, Wilaya ya Magharibi ‘B’ Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, ndipo watuhumiwa hao walifanya mbinu na walifanikiwa kuwaiba.

Aidha alisema Jeshi hilo linaendelea na upelelezi wake, ili kuhakikisha wanafanikiwa kusitisha matukio wizi wa mifugo, na baada ya kukamilisha upelelezi watuhumiwa hao watafikisha Mhakamani. 

Katika hatua nyengine Jeshi la Polisi Mkoa Mkoa huo, linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za kupatikana na dawa za kulevya.

Kamanda huyo Alisema watuhumiwa hao ni Mohammed Salum Abdi (24) mkaazi wa Fuoni Mambosasa, Rashid Issa Lulungu (22) mkaazi wa Kihinani, Ali Ahmada Haji (20) mkaazi wa Mambosasa.

Alisema watuhumiwa hao wamekamatwa Julai 28, hadi Agosti 3 mwaka huu, katika maeneo tofauti ya Mkoa huo wakati wa wa operesheni za kupambana na uuzaji na utumiaji wa dawa za kulevya.

Aidha alisema vijana hao walikamatwa na mafurushi mawili ya majani makavu na nyongo 76 wakiwa wanajihusisha na vitendo vya utumiaji wa dawa za kulevya, katika maeneo hayo wakati jeshi hilo likiwa kwenye doria zake za kusaka wahalifu.

“Ni jukumu letu kuwalinda wananchi pamoja na mali zao juu ya matukio ya kihalifu yanayofanywa hapa nchini” alisema.

Kamanda alisema, jeshi hilo linaendelea na upelelezi kwa watuhumiwa hao, baada ya kukamilika watafikishwa katika vyombo vya sheria.

Hivyo aliwaomba vijana wanaojishulisha na tabia ya kuuza au kutumia dawa za kulevya kuaacha haraka, kwani jeshi hilo linaendelea kupambana na limeweka mikakati maalum kwa kuzuia wasambaji wa dawa za kulevya nchini. 

Mbali na hayo alisema jeshi la Polisi litaendelea na operesheni zake mara kwa mara kwa lengo la kuimarisha ulinzi katika mkoa wake na kuwaomba wananchi kushirikiana katika kuwafichua wahalifu ambao hawana dhamira njema na nchi yao ikiwemo wauzaji wa dawa za kulevya ambao wanaharibu nguvu kazi ya taifa.