NA TATU MAKAME
WAFANYABIASHARA wa nguo na vinyago katika eneo la Forodhani Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, wamesema bado hali ya mauzo hairidhishi licha ya ugonjwa wa corona kupungua nchini.
Wafanyabiashara hao walisema hayo kwa nyakati tofauti wakati wakizungumza na Zanzibar Leo, ambapo alisema licha ya harakati za utalii kuanza na wageni kuingia nchini, lakini hali ya biashara kwa bidhaa hizo hairidhishi ingawa wapo wageni wanaotembelea madukani kuona bidhaa zao.
Walisema wakati dunia ilipokubwa na ugonjwa huo walilazimika kufunga maduka kwa kipindi cha miezi minn,e lakini baada ya kurudi harakati hizo kumekuwa na wateja ni wachache.
Doto Charless Mazuku, alisema wageni wanaotoka nje ya nchi wengi wanatembea tu kwenye maduka na sio kununua hali inayopelekea biashara kuwa nguvu.
Humudi Saidi Ahmed alisema kukosa kwa wateja kumepelekea kukosa pesa za kuendesha maisha na kulipa kodi ingawa serikali inategemea kulipwa kodi, lakini biashara hailipi kutokana na kukosa wateja.
“Tunaiomba serikali ipunguze kodi biashara yetu imesita kwa muda mrefu”,alisema.
Joile Tomas Mwakibinga ni mmoja wa wafanyabiashara wa nguo na vinyago, alisema hali ya biashara bado ni ndoto kutokana na kukosa wateja wa uhakika wanaohitaji bidhaa hizo.
”Sasa ni 15% tu ya wateja ndio wanaofika kutaka huduma na wengi wao ni wateja wa ndani ikiwemo Tanzania bara”alisema mfanyabiashara huyo.
Akizungumzia kuhusu kodi mfanyabiashara huyo, alisema walisamehewa kulipa kipindi cha ugojwa wa corona baada ya kupeleka maombi ya msamaha.
“Sisi tulisamehemwa maana tumekodishwa na mtu binafsi na hali alikuwa anaiona lakini wenzetu walilipa na wanamalalamiko makubwa ya kulipa kodi”,alisema.
Akizungumzaia malipo ya wafanyakazi kwa kuwalipa nusu mishahara kwa kipindi hiki alisema imewalazimu kuwaeleza hali halisi waliyonayo kwani hukusanya shilingi 100,000 kwa siku mbili hadi 200,000.
Meneja Uhusiano huduma kwa walipa kodi kutoka bodi ya mapato (ZRB) Shaabani Yahya Ramadhani alisema serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia bodi ya mapato Zanzibar (ZRB) imepunguza kiwango cha utoaji wa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kutoka asilimia 18 hadi asilimia 15.
Meneja huyo alisema hayo hivi karibuni katika mafunzo yaliyowashirikisha waandishi wa habari kuhusu marekebisho ya sheria za kodi kwa mwaka 2020/2021, ambapo sheria zilizofanyiwa marekebisho ni pamoja na sheria ya usimamizi wa kodi (TAPA), sheria ya ongezeko la thamani (VAT),sheria ya ushuru wa hoteli, sheria ya rufaa za kodi Zanzibar.
Mkurugenzi Masoko kutoka Kamisheni ya Utalii Zanzibar Miraji Ukuti Ussi, alisema mikakati yao kuhakikisha watalii wanaingia kwa wingi nchini baada ya harakati za kitalii kurudi.