NA   TAKDIR ALI, MAELEZO

VIJANA nchini wametakiwa kuuendeleza umoja na mshikamano uliopo nchini, kwani kuna maisha baada ya kumalizika zoezi la uchaguzi mkuu.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Magharibi kichama Mohammed Rajab Soud, alieleza hayo alipokuwa akifungua mkutano wa kuwachagua mwakilishi na mbunge wa viti maalum kupitia Umoja wa Vijana ndani ya Mkoa huo.

Alisema vijana wana mchango na thamani kubwa katika chama na taifa kwa ujumla, hivyo ni vyema kurudi katika hali ya kawaida mara baada ya kumaliza uchaguzi huo wa kura za maoni.

Alisema si wakati wa kutengeneza makundi ambayo yataiathiri jumuiya hiyo na wengine kubakiwa na madukuduku rohoni na kwamba CCM inasonga mbele kutokana na umoja.

Mwenyekiti huyo aliwaeleza vijana hao kwamba uchaguzi isiwe ni chanzo cha kuwatenganisha na kuwagombanisha kwani kitendo hicho kinaweza kuleta mpasuko katika chama na jumuiya zake.

Kwa upande wake msimamizi mkuu wa uchaguzi huo ambae pia ni mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Ayoub Mohammed Mahmoud amewataka walioongoza katika uchaguzi huo kuzingatia maadili ya chama ili kujiepusha na matatizo yanayoweza kujitokeza.

Katika uchaguzi huo wajumbe wa baraza kuu la Umoja wa Vijana Mkoa wa Magharibi wamemchaguwa Salma Abdullah Haji kwa upande wa ubunge na Thuwaiba Jeni Pandu kwa uwakilishi kupitia umoja wa vijana wa mkoa wa Magharibi.