NA ABOUD MAHMOUD

MABINGWA wa ligi kuu kanda ya Unguja kwa mchezo wa mpira wa Kikapu, Stone town, wamejigamba kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya Zanzibar mara baada ya kukutana na mabingwa wa kanda ya Pemba.

Akizungumza na gazeti hili,kocha wa timu hiyo Fuad Rashid Omar mara baada ya kuibuka na ubingwa huo kwa kuwalaza Nyuki kwa magoli 63-52 katika uwanja wa Mao Zedong hivi karibuni.

Kocha huyo alisema wanatarajia timu itakayochukuwa ubingwa kisiwani Pemba watakuja Unguja kuvaana nao mnamo Septemba 5 mwaka huu .

“Ubingwa tulioupata msimu huu wa kanda ya Unguja tuna matumaini makubwa ya kuchukua na wa Zanzibar kwa ujumla kutokana na tulivyojipanga baina yetu viongozi na wachezaji,”alisema kocha huyo.

Fuad alisema wamejipanga kufanya mazoezi kama kawaida ili kurekebisha makosa madogo yaliojitokeza ikiwemo yale ya kiufundi zaidi .

Alifafanua maeneo ambayo watajitahidi kuyafanyia mazoezi ili waweze kufanya uzuri ikiwemo wakati wa kushambulia  na kutambua wacheze vipi ili wasiweze kufungwa.

“Hivi sasa tunajipanga kuanza mazoezi ambayo yatafanya katika mchezo wetu na timu kutoka Pemba kuchukua ubingwa,kwani wachezaji wako tayari kimazoezi na tukiangalia Septemba 5 haiko mbali,”alifafanua.