BILA ya shaka yoyote ile kuanzishwa kwa taasisi za kitaaluma kama vile vyuo vikuu lengo lake ni kuiwezesha nchi kunufaika kwa kuzalisha wataalamu ambao ndio chachu ya tafiti zinazogusa moja kwa moja maendeleo na ustawi wa wananchi kiuchumi na kijamii.

Kwa maana hiyo, kuimarika kwa uchumi wa nchi na kuimarika kwa hali za maisha ya watu kunategemea zaidi kipaumbele kinachotolewa katika taaluma, mwamko pamoja na utayari wa Serikali na wana jamii kutumia matokeo ya tafiti zilizo rasmi kwa faida yao na nchi. 

Vile vile malengo hayo yatafikiwa iwapo tutakuwa na udadisi pamoja na ujasiri wa kutaka kujua wenzetu ambao tunalingana kimazingira yaani maliasili na vivutio vyetu na nchi hizo za wenzetu waliwezaje kufanikiwa na sisi tukabaki nyuma. 

Katika serikali ya Mapinduzi Zanzibar ni dhahiri utafiti umepewa umuhimu wa mbele kwa sababu kila wizara imeundiwa Kurugenzi za Sera, Utafiti na Mipango. Isingefanya hivyo iwapo haitilii maanani suala la umuhimu wa tafiti kwa ustawi wa nchi na watu wake.

Kwa upande mwengine wito umekuwa ukitolewa kwa wasomi, taasisi za kimaendeleo na wataalamu wa Zanzibar kuwa na kawaida ya kufanya tafiti mara kwa mara, zitakazosaidia kuinua hali za maisha ya wananchi.

Katika mazingira ya Zanzibar ambapo kilimo, kikiwemo cha mwani na karafuu, kina nafasi ya kipekee katika kuiingizia mapato nchi na kutoa ajira nyingi kwa wananchi, wakiwemo akinamama, hasa wale wa maeneo ya vijijini, tafiti za mazao ya kilimo hatuwezi kuziepuka kama kweli tunataka maendeleo ya wananchi wetu na nchi.

Kwa sababu serikali inaelewa hilo, huenda ndio maana hadi sasa inasemekana kuwa sekta ya kilimo ndiyo inayoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wataalamu hapa Zanzibar.

Wingi huo unawafanya watu wajiulize wataalamu wa kilimo, mifugo na uvuvi mbona haujaendena na mafanikio yaliyotarajiwa katika sekta hizo? 

Lililo wazi ni kuwa utafiti mara zote hujumuisha matumizi makubwa ya fedha na rasilimali nyengine kama dhamira yetu ni kweli kunufaika na matokeo yake, ni bora nikumbushe mapema kuwa, bajeti za Serikali, Jumuiya na hata washirika wa Maendeleo hazinabudi kufanywa nono katika kufanikisha tafiti.