NA TATU MAKAME

WANANCHI na wanafunzi  wanaokwenda kupumzika katika bustani ya Jamuhuri Gaden iliyopo mbele ya Skuli ya Haile Selassie, wamesema tabia inayofanywa na baadhi ya watu kutupa taka ndani ya bustani ni kuharibu madhari na si kitendo cha uungwana.

Wananchi hao walisema hayo kwa nyakati tofauti wakati walipozungumza na mwandishi wa habari  kufuatia kuwepo kwa watu wanaotupa taka eneo hilo.

Walisema licha ya Baraza la Manispaa Mjini kuweka makontena ya taka kila eneo la makaazi na sehemu za mapumziko, lakini bado watu  wanaotupa taka ovyo na kupelekea kuharibu mazingira kwa makusudi.

 “Wanapojitokeza wananchi kutupa taka eneo hili wanaharibu taaswira nzima ya bustani na hili ni eneo la mapumziko lakini utaona wapo watu wanatupa taka” walisema.

Ali Mohamed Juma, kutoka Sogea, ambae alifika sehemu hiyo kwa ajili ya mapumziko wakati wa jioni  alisema kitendo cha kutupa taka eneo la bustani ni kuharibu mazingira hasa ukizingatia umuhimu wake.

 “Bustani yetu imekuwa kivutio kikubwa kila mgeni anaefika Zanzibar hupendelea kuja eneo hili kwa ajili ya mapumziko hivyo suala la kutupwa taka ni kuonyesha dharau kwa bustani hii”,alisema.

Nae Fatma Iddi Hassan kutoka Kwaalinato alisema kitendo cha kutupa taka eneo hilo sio tabia nzuri hivyo aliliomba Baraza la Manispaa mjini kusimamia eneo hilo ili kuzuia hali hiyo.

“Kama kutawekwa walinzi wa kuangalia watu wanaotupa taka katika eneo hili itapendeza zaidi kuliko watu kuachiwa kuharibu mazingira kwa makusudi”,alisema.

Nao wanafunzi wa  vyuo vikuu ambao hawakupendelea kutajwa majina yao Gazetini walisema mategemeo yao ni kuona sehemu hiyo inabakia safi kwani wanaitumia kwa kudurusu masomo yao hasa wakati wanapokabiliwa na mitihani ya taifa na wameomba kusimamiwa eneo hilo.

Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa Mjini, Saidi Juma Ahmada, alikiri kuwepo watu wanaotupa taka eneo hilo na wanaendelea kufanya usafi ili kuhakikisha mji unabakia katika hali nzuri na kuwataka wananchi wenye tabia ya kutupa taka eneo hilo kuacha, kwani wanaharibu haiba ya mji.