NA JAMES K. MWANAMYOTO, DODOMA
KURUGENZI ya Intelijensia ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imedhamiria kuimarisha utekelezaji wa operesheni za kiuchunguzi za TAKUKURU dhidi ya vitendo vya rushwa vinavyojitokeza kwa maana ya ufuatiliaji na uchakataji wa taarifa za kiintelijensia zinazopatikana kutoka katika maeneo mbalimbali kwa lengo la kutokomeza vitendo vya rushwa nchini.
Hayo yamesemwa jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Kapt. (Mst) George H. Mkuchika, wakati akitoa neno la utangulizi kumkaribisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa Majaliwa, kuzindua jengo la Ofisi ya Intelijensia ya TAKUKURU lililojengwa Makao Makuu ya Nchi Dodoma.
Mkuchika amefafanua kuwa, jengo hilo ni muhimu sana kwa Serikali ambayo imedhamiria kwa dhati kutokomeza vitendo vya rushwa nchini, kwani litatumiwa ipasavyo na watumishi wa Kurugenzi ya Intelijensia ya TAKUKURU kufanya uchunguzi makini, ufuatiliaji wa kina na kuchakata taarifa za kiintelijensia kwa weledi.