KABUL, AFGHANISTAN

KUNDI la wanamgambo la Taliban limesema  kuwa, liko tayari kufanya mazungumzo ya amani na Serikali ya Afghanistan,baada ya kufikiwa makubaliano ya kubadilishana wafungwa, ambapo maofisa wanasema zoezi hilo litaanza siku mbili zijazo.

Maelfu ya viongozi muhimu wa Afghanistan walikubaliana kuachiwa kwa mamia ya wafungwa wa Taliban, wanaotuhumiwa kwa makosa makubwa na hivyo kuondoa kizuizi muhimu katika kuanza kwa mazungumzo ya amani.

Msemaji wa Taliban Suhail Shaheen,lisisitiza kuwa msimamo wao uko wazi, endapo zoezi la kuwaachia wafungwa litakamilika, basi wako tayari kuanza mazungumzo huku duru ya kwanza ya majadiliano ikitarajiwa kufanyika mjini Doha, Qatar.

Suala la kubadilishana wafungwa lilikuwa sehemu muhimu ya mkataba wa amani uliofikiwa mwezi Februari, ambao ulishuhudia Marekani ikikubali kuwaondoa wanajeshi wake nchini Afghanistan.