NA ASYA HASSAN

CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) Zanzibar, kimesema kitaendelea kuwasaidia wanawake, ili waweze kujiongezea kipato na kujipatia maendeleo.

Ofisa uwezeshaji wanawake kiuchumi kutoka TAMWA, Nayrat Abdalla Ali, alisema hayo alipokuwa akizungumza na wajasiriamali waliyoshiriki hivi karibuni katika maonesho ya nane nane huko Dole.

Alisema ili wanawake waweze kujisaidia wenyewe wanahitaji kuungwa mkono katika nyanja zote, hivyo chama hicho kimekuwa mstari wa mbele katika kusimamia miradi kadhaa pamoja na kuwapa elimu na mbinu tofauti, ili waweze kujikwamua kiuchumi na kuondokana na umaskini.

Akizungumzia juu ya wajasiriamali hao kushirika katika maonesho afisa huyo alisema maonesho hayo yamewasaidia kujitangaza, kuongeza ujuzi pamoja na kupata taaluma na mbinu mpya ya kuzalisha na kuuza bidhaa zao.