NA FARIDA MSENGWA, MOROGORO
WAHARIRI wa vyombo vya habari nchini kuelimisha wananchi na mafanikio ya kupamba na umaskini yaliyopatikana kupitia mpango wa kunusuru kaya masikini unaosimamiwa na mfuko wa maendeleo ya jamii Tanzania (TASAF).
Hatua hiyo ikiwa ni pamoja na kutumia vyema fursa iliyotolewa na serikali kupitia TASAF ili kasi ya kupambana na umasikini nchini iendelee kuwa ya mafanikio.
Rai hiyo, ilitolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Loata Sanare wakati wa ufunguzi wa kikao kazi kwa Wahariri wa vyombo vya habari kuhusu utekelezaji wa kipindi cha pili cha awamu ya tatu ya TASAF, katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Katibu Tawala wa mkoa huo Injinia Emanuel kaluvelo.
Alisema lengo kuu la kikao kazi hicho ni kujengea uelewa kuhusu utekelezaji wa TASAF awamu ya tatu, kutokana na uwezo na nguvu ya vyombo vya habari katika kuwafikia wananchi kwa wingi na haraka.
Alisema kuwa elimu hiyo, itasaidia kuongeza uelewa wa jamii na kuwafanya wanufauika waliofanya vizuri katika awamu zilizotangulia kujiondoa kwenye mpango huo.
Aliongeza kuwa, mpango huo umekuwa kichocheo kikubwa kilichowafanya baaadhi ya wanufaika waondoke kwenye umasikini uliokithiri na kuondolewa katika mpango jambo ambalo ndio lengo la kuanzishwa kwa mpango wa TASAF.
“Tangu kuanzishwa kwa Mfuko wa maendeleo ya jamii TASAF takribani miaka 20, miradi mingi imetekelezwa kwa ufanisi, jambo lililoendelea kuifanya serikali kuuamini na kuupa tena mfuko huo majukumu mengi zaidi ya kusaidia jitihada za kuwaondolea wananchi kero ya umasikini,” alisema Sanare.
Aidha sanare alivipongeza vyombo vya habari na wanahabari nchini kwa kuendelea kutoa habari za maendeleo jambo linalochochea ukuaji wa uchumi wa nchi na kaya mojamoja.
Mkurugenzi wa TASAF Ladislaus Mwamanga, alisema toka kuanzishwa kwa mpango huo, jumla ya miradi 1,704 ilitekelezwa kwa jamii yenye thamani ya shilingi bilioni 72 katika hamashauri 40 za Tanzania bara na Zanzibar ambapo miradi 1,338 ni ya huduma za jamii, miradi 61 makundi maalumu pamoja na miradi 305 ya kutoa ajira za muda.
Mwamanga alieleza kuwa katika utekelezaji wa mpango huo, tasaf imekuwa ikitoa ruzuku kwa wanufaika na kwamba zimewasaidi kupata mahitaji ya msingi ikiwemo chakula,vifaa vya skuli kwa watoto na kuanzisha miradi midogomidogo ya kujiongezea kipato.
“Hali hiyo imeongeza utulivu katika kaya lakini mahudhurio ya watoto shuleni na kliniki yameongezeka kwa sababu wazazi wameweza kutimiza mashariti ya elimu pamoja na afya,” alisema Mwamanga.
Aidha mwenyekiti wa kikao kazi hicho, mwandishi mwandamizi wa magazeti ya uhuru na mzalendo Celina Wilson mbali ya kumshukuru mkuu huyo wa mkoa na viongozi wengine, aliupongea uomngozi wa TASAF kwa kuona umuhimu wa kutoa elimu kwa wanahabari juu ya shughuli za mfuko huo.
“Tunaamini tutakapoondoka hapa tutakuwa na ziada ya taarifa za juu ya shughuli za TASAF, mafanikio na changamoto mnazokabialiana nazo jambo ambalo litasaidia kuchangia utatuzi wake kupitia vyombo vyewtu vya habari,” alisema Celina.
Awali mkuu wa mtaalamu wa mawasiliano wa mfuko huo, zuhura mdungi alieleza kuwa kikao hicho kitafuatiwa na vyengine vitakavyohusisha waandishi wa habari ambao watapatiwa mafunzo na kupata fursa kukagua utekelezaji wake katika maeneo mbali mbali nchini.
Katika kikao hicho, waandishi na wahariri hao walipata nafasi ya kutembelea vijiji vya Lubungo ‘A’ na Gwata, kata ya Mikese, wilaya ya morogoro vijijini na kuwashuhudia wanufaika wa mpango huo jinsi walivyopiga hatua za maendeleo ikiwemo ya kuimarisha makaazi yao na elimu kwa watoto wao.